Friday 7 February 2014

Mwigulu: Sheria ya Ununuzi wa Umma wizi wa kistaarabu

Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba ametoboa madudu aliyoyaona kipindi kifupi alichokaa kwenye ofisi hiyo baada ya kuapisha hivi karibuni.
Alisema amegundua sheria ya ununuzi ni uchochoro wa wizi wa kistaarabu unaotishia ustawi wa taifa.
Mwigulu alisema ni wizi wa kutisha kuona mtu binafsi akinunua soksi dukani analipa Sh2,000, lakini akitumia sheria ya ununuzi soksi ya aina ileile itanunuliwa kwa Sh80,000.
Alisema sheria hiyo ni mzigo mzito kwa Serikali na kutoa mfano mwingine kwamba, waziri mmoja alikwenda safari ya kikazi nje ya nchi, lakini aliamua kwenda na mkewe kwa gharama zake alimlipia Sh1 milioni, lakini yeye kwa utaratibu sheria ya ununuzi alilipiwa na Serikali tiketi ya Sh4 milioni wakati walikuwa ndege moja na viti vinavyofuatana.
Mwigulu alisema hayo juzi jioni alipozungumza na wafanyabiashara jijini hapa kupitia Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), huku wakimweleza kuwa sera mbaya ya kodi ndiyo inayosababisha watu wengi kukwepa ulipaji kodi.
‘Nakiri kwamba kweli ipo haja ya kurekebisha sheria ya kodi na sera yake, kutokana na mambo ninayoyaona na yatafanyiwa kazi kipindi kifupi kijaacho,’’ alisema.
Mwigulu alisema kwa kuanza utekelezaji, tayari amewaagiza maofisa wa wizara wamwandalie orodha ya misamaha ya kodi na wahusika wake muda wa miaka mitano. Pia, ameagiza kupatiwa orodha ya walipa kodi wakubwa na jinsi wanavyolipa.
“Pia, nimewataka wanipe orodha jinsi zilivyolipa kodi kampuni kubwa zinazobadili majina kila baada ya muda fulani, hususan za simu ili kujua wanavyolipa kodi,” alisisitiza.
Naibu waziri alisisitiza kwamba Sera ya Kodi imesababisha kuanzishwa kwa sheria ya ununuzi ambayo nia yake ilikuwa nzuri, lakini sasa imekuwa kichaka cha wizi wa kistaarabu na itarekebishwa.
Kuhusu umuhimu wa mashine ya elektroniki, alisema yeye ni muumini wa mashine hizo kwamba ipo haja kwa wafanyabiashara wote kuielewa vizuri ili waweze kuona faida zake na kwamba, itawaondolea usumbufu.
Wakurugenzi wa halmashauri waonywa
Awali juzi asubuhi, Mwiguli alizungumza na wakurugenzi wa halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya kwenye Ukumbi wa Mkapa ambapo aliwataka kuacha mara moja mambo ya ufisadi na kuwataka kusimamia kwa akili fedha hizo ili kukwepa jela.

Mwananchi

No comments:

Post a Comment