ANAITWA Ramadhan Hassan Masanja, lakini sisi watu wa burudani tunamfahamu zaidi kama Banza Stone, Le general, yule kijana wa Sinza jijini Dar es Salaam mwenye kipaji kisicho na shaka katika muziki wa dansi Tanzania.
Ukiondoa muziki wa dansi uliokuwa ukipigwa na Bendi za Marquis, OSS, Vijana Jazz, Dar International, Tancut Almas, Juwata Jazz, Washirika, DDC Mlimani, Bantu Group na nyingine za enzi hizo, Banza ni jina kubwa kabisa miongoni mwa vijana waliokuja kuleta mageuzi makubwa ya muziki huo uliotawaliwa na sebene za Kikongo.
Kuanza kutaja safari ya Banza Stone katika muziki wa dansi itakuwa ni sawa na kejeli, kwani historia yake haiwezi kutosha katika sehemu hii ndogo, lakini itoshe tu kusema kuwa mchango wa mwanamuziki huyu ni mkubwa, wenye kutukuka na unaostahili kuenziwa.
Ni mwenye kipaji na anayejua kukitumia. Anajua kutunga, anajua kuimba, ni mtoto wa mjini. Nini zaidi?
Wakati fulani Banza alichukuliwa na TOT Plus, akitokea African Stars ‘Twanga Pepeta’ ambako yeye alikuwa ndiye mwimbaji nyota na kiongozi. Hii bendi ya CCM, haikuwahi kuwa juu kabla, zaidi alikuwa ni Malkia wa Mipasho, Khadija Omar Kopa ndiye aliyekuwa akitamba na kundi lake la taarabu.
Banza aliipaisha TOT Plus kiasi cha kuweza kuwa tishio kubwa kwa Twanga Pepeta na muziki wa dansi kwa jumla. Kumbukumbu zinaonyesha bendi hiyo ilianza kurejea ilipokuwa baada ya kuondoka kwa mkali huyo wa kibao kilichotamba sana, Angurumapo Simba.
Ngoja nikupe kitu cha kusisimua kuhusu Banza. Alipoondoka TOT, alirejea tena Twanga, wakati huo Ally Choki akiwa Mchinga Sound. Kuna kibao kimoja kinaitwa Mtu Pesa alikitunga na kuimba Banza Stone.
Ndani yake kuna mashairi yaliyoimbwa kwa kuchukua baadhi ya mistari ya kwenye Biblia. Sasa siku moja nilikutana na Kapteni John Komba ofisini kwake. Kumbuka huyu ndiye Mkurugenzi mtendaji wa kundi hili la propaganda la chama tawala. Alikuwa akimlalamikia Banza kwa ‘kuiba’ mashairi yake.
“Banza alikuja hapa ofisini kwangu, akaona hii fremu hapa (Komba anaonyesha fremu yenye maneno ya dini ya Kikristo ofisini kwake) akachukua haya maneno akaenda kuimba ule wimbo. Ameniwahi kwa sababu nilikuwa nataka kuyatumia,” alisema John Komba!
Ni kwamba Banza alikwenda ofisini kwa bosi wake, akakuta maandishi yenye maana ukutani, akayachukua na kuyafanyia kazi, lakini aliyeyaweka hakudhani kama angeweza kutoa burudani kwa maneno yenye hekima kama yale!
Lakini kuna jambo moja Banza Stone analikosea. Umaarufu wake umempoteza njia sahihi ya kufuata katika maisha, amepitia katika vichochoro vya mateja badala ya red carpet ya masupastaa.
Banza Stone anadaiwa kutumia unga kama alivyokuwa nyota mwingine Msafiri Diouf na mnenguaji Aisha Madinda. Hivi sasa, habari zinasema nyota huyu anaumwa. Hii siyo mara ya kwanza kwake kuandamwa na maradhi. Lakini kitu kinachoumiza ni kwamba kila anapopata nafuu, anarejea tena tabia yake ya ulevi.
Dunia ya burudani ingependa sana kumsaidia Banza Stone, iwe kwa matibabu au ushauri, lakini tatizo linakuja kwamba yeye mwenyewe haonyeshi kama anahitaji msaada. Ni kama aliyeridhika na kinachomtokea. Wakati mwingine mtu anaweza kuwalaumu ndugu, marafiki au majirani kwa kutomjali, lakini ukweli ni kwamba ni yeye mwenyewe ndiye anayetengeneza taswira mbaya juu yake.
Muziki wa dansi bado unamhitaji Banza Stone, sanaa ya burudani bado ina vitu muhimu kutoka kwake. Anapaswa kutambua thamani yake halisi na kuachana na mambo yasiyo na faida. Ujana una mambo mengi na haya ndiyo yanayomtokea.
Lakini kijana ambaye hakui ana matatizo. Vijana wengi walivuta bangi wakiwa mashuleni, lakini leo wameacha kwa sababu siyo wakati wao tena. Kuna vitu visivyo vya lazima ambavyo nyota huyu anapaswa kuviacha hasa kutokana na umri wake!
No comments:
Post a Comment