Matumizi ya dawa za kulevya nchini yamechukua sura mpya, baada
ya kubainika kuwa watumiaji wengi wa dawa hizo aina ya heroin na cocaine
sasa wanatumia dawa za hospitali zenye uwezo wa kulevya kuwa mbadala.
Matumizi hayo mabaya yamebainika kutokana na
kuwapo ongezeko la matumizi ya dawa za hospitali zilizo na nguvu
inayoelezwa kulingana na dawa za kulevya ikiwamo heroin, cocaine na
amphetamine.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya Uhalifu na Dawa za
Kulevya (UNODC) ya mwaka 2013, inathibitisha ongezeko hilo la matumizi
ya dawa hizo, ambazo kitaalamu zinaitwa ‘new psychoactive substances
(NPS).
“Dawa mbadala za dawa za kulevya zimezua wasiwasi
mkubwa siyo kwa sababu ya ongezeko la matumizi yake, bali hata ukosefu
wa utafiti wa kisayansi na uelewa wa matumizi yake,” ilisema sehemu ya
ripoti ya UNODC.
Katibu Mkuu UNODC, Yury Ferdotov alieleza katika
ripoti hiyo ya hali ya dawa za kulevya mwaka 2013 kwamba, changamoto
kubwa iliyopo katika kudhibiti dawa hizo duniani ni matumizi ya dawa za
hospitali na kemikali zinazotumika kuzitengeneza kutumika kama dawa za
kulevya.
Alisema nchi nyingi duniani hazina sheria wala
uelewa kuhusu kemikali hizo, jambo linalosababisha wafanyabiashara
wakubwa kuendelea kusafirisha kemikali hizo au kutumia teknolojia kulima
mimea inayotumika kutengeneza dawa hizo.
UNODC limefafanua kuwa matumizi mabaya ya dawa
hutokea wakati dawa za hospitali zinapotumika kwa malengo mengine
kinyume na tiba.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa aina tisa
ya dawa za hospitali ni miongoni mwa dawa zinzouzwa kwa njia ya panya
kama mbadala wa heroin na cocaine.
Dawa hizo ni pamoja na mephedrone, ketamine, benzodiazepine, tramadol na dextromethorphan.
Nyingine ni piperazines, phencyclidines, trypitamines na aminoindance.
Uchunguzi huo umebainisha kwamba unaweza kuzipata
dawa hizo kwa wafamasia wasio waaminifu katika hospitali kubwa ambapo
huuzwa kwa bei nafuu na wakati mwingine katika maduka ya dawa muhimu.
Mwananchi Jumamosi lilipita katika baadhi ya
maduka ya dawa na kufanikiwa kuzinunua dawa hizo zilizothibitishwa
kutumika mbadala wa dawa za kulevya bila ya kuwa na cheti cha daktari.
Chanzo Mwananchi
Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment