Tuesday, 29 October 2013

Watumishi wa umma kulipwa kulingana na elimu

SERIKALI imepanga kutengeneza miongozo itakayowapanga watumishi wa umma katika makundi mbalimbali kwa ajili ya kulipwa kulingana na elimu yao.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Mtendaji wa Bodi ya Mishahara na Maslahi wa Ofisi ya Rais, Tamika Mwakahesya, baada ya kuapishwa na Rais Jakaka Kikwete kushika wadhifa huo.
Mwakahesya alisema hiyo itakuwa kazi yake ya kwanza ikifuatiwa na utafiti kuhusu vyanzo vya makusanyo nchini ambavyo vinawezesha watumishi wa umma waweze kulipwa.
“Kutokana na hali halisi ya uchumi ulivyo nchini na hasa ikizingatiwa kwamba mishahara ya watumishi inahitaji makusanyo inanipasa niangalie vyanzo vya makusanyo yetu kabla ya kuongeza au kupunguza mishahara,” alisema. Mwakahesya ambaye kabla ya wadhifa huo alikuwa Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Kazi na Ajira, aliwataka watumishi wa umma kutofanya kazi kwa mazoea bali wafanye kwa tija, ili kipato chao kiweze kuboreshwa.
Naye Daniel Ole Njoolay ambaye aliapishwa na Rais Kikwete kuwa Balozi wa Tanzania nchini Nigeria na nchi zilizo Magharibi mwa Afrika alisema atatumia nafasi aliyoteuliwa kuzishauri nchi kuja kuwekeza na kutalii.
“Namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kunikumbuka …wakati nastaafu ukuu wa mkoa wa Rukwa mwaka 2011 aliniahidi kunipangia kazi nyingine, sasa amenipangia hivyo nitafanya kazi bila kuchoka,” alisema.
Katika hafla ya kuwaapisha viongozi, Rais Kikwete pia alimwapisha Bashir Mrindoko kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji na Raphael Daluti kuwa Naibu Katibu Mkuu katika wizara hiyo.

No comments:

Post a Comment