Kuna uwezekano wa kuzuka mvutano mkali kwenye Mkutano wa 13 wa Bunge unaoanza leo mjini Dodoma kutokana na utata wa maandalizi ya Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni unaotakiwa kuwasilishwa.
Mijadala ya miswada miwili, ambayo inahusiana na 
mchakato wa kupata Katiba Mpya ndiyo inatazamiwa kuwasha moto katika 
Bunge hili.
Miswada inayosubiriwa kwa hamu ni pamoja na ule wa
 Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na ule wa 
Sheria ya Kura ya Maoni.
Maandalizi ya Muswada wa Kura ya Maoni huenda 
yakazua zogo bungeni kutokana na kuwapo malalamiko kuwa upande wa 
Zanzibar haukushirikishwa kikamilifu.
Pia inasemekana Kamati ya Haki, Sheria na Utawala haijakaa kupitia muswada huo na pia haijakutana na wadau mbalimbali.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, aliiambia Mwananchi kuwa hawajaupitia muswada huo baada ya kufanyiwa marekebisho.
Akizungumzia suala hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya 
Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi alisema muswada 
huo uliondolewa kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho ambayo alieleza kuwa 
tayari yameshafanyika.
“Muswada sio kama uliondolewa bila kujadiliwa, 
ulijadiliwa na baadaye tulikubaliana ufanyiwe marekebisho ambayo tayari 
yameshafanyika. Wiki hii tutauwasilisha tena mbele ya Kamati,” alisema 
Lukuvi.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, 
Sheria na Utawala, Pindi Chana kueleza kama Kamati hiyo ilikutana na 
upande wa Zanzibar alisema, “Siwezi kuzungumzia suala la miswada na 
gazeti lenu (Mwananchi), sitaki kueleza lolote, kama unataka maelezo 
mtafute Katibu wa Bunge au Spika,” alisema na kukata simu.
Muswada huo unaeleza kuwa kura ya maoni inatakiwa 
kupigwa Tanzania Bara na Zanzibar, jambo ambalo lilipingwa na upande wa 
Zanzibar kwa madai kuwa nao wana sheria kama hiyo na kwamba masuala ya 
kura ya maoni siyo ya Muungano
Muswada wa Sheria ya Marekebisho
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu 
Mkurugenzi wa Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa wa Bunge, 
Deogratias Egidio alisema kuwa pamoja na miswada hiyo miwili pia 
kutakuwa na miswada zaidi
Egidio alisema muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya 
Mabadiliko ya Katiba unatarajiwa kurudishwa bungeni baada ya kuombewa 
hati ya dharura.
Alikiri kuwa bado walikuwa hawajapelekewa, lakini wanategemea wakati wowote utapelekwa bungeni.
Muswada wa magazeti
Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali 
unatazamiwa kuwa moto kwani utalenga kurekebisha sheria mbalimbali 
ikiwamo Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976.
Wabunge tayari wamepigia kelele marekebisho hayo na Chadema wametoa tamko rasmi kuupinga.
Katika ya marekebisho ya muswada huo ni 
kupendekezwa kuongezwa faini kutoka Sh150,000 hadi Sh5 milioni kwa 
magazeti yatakayoandika habari za uchochezi, huku kipengele cha 
kufungiwa kwa magazeti kikiachwa kama kilivyo.
No comments:
Post a Comment