Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kama kitapewa ridhaa ya
kuongoza nchi mwaka 2015, watabadilisha matumizi ya Ofisi ya Spika
iliyojengwa na mbunge wa Urambo Mashariki, Bw. Samuel Sitta.
Akizungumza
juzi katika mkutano wa hadhara wilayani humo, mkoani Tabora, Mkurugenzi
wa Kampeni na Uchaguzi wa chama hicho, Msafiri Mtemelwa, alisema ofisi
hiyo wataibadilisha kuwa wodi ya wazazi ili iweze kuwasaidia wanawake
wanaoteseka kupata huduma ya afya.
Alisema Bw. Sitta alijenga jengo hilo ili litumike kama ofisi ya Spika
wa Bunge kabla ya kumaliza muda wake wakati mji huo hauna barabara za
lami wala hospitali za kutosha hivyo kama watapewa ridhaa, watalibadili
matumizi yake.
Alisema Mkoa huo una historia kubwa nchini lakini hauna maendeleo
ambapo badala ya Serikali kujenga barabara nzuri na kuwapa wananchi maji
safi na salama, Bw. Sitta alijenga ofisi akiamini hata ondoka katika
kiti hicho.
"Sitta amekuwa mbunge tangu 1976 katika jimbo hili lakini hadi leo
hakuna barabara za lami mjini wala zinazoingia na kutoka katika jimbo
hili," alisema Mtemelwa..Aliongeza
kuwa, miaka ambayo Bw. Sitta amekuwa mbunge wa jimbo hilo inamtosha
hivyo ni lazima wananchi wachague mbunge kutoka upinzani ambaye
hataogopa kusema ukweli ili kuharakisha maendeleo yanayohitajika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kanda ya Magharibi inayoundwa na Mikoa
ya Katavi,Tabora na Kigoma, Bw. Shabani Mambo, alisema kwa muda mrefu
wakazi wa Kigoma walikuwa wakikichagua Chama Cha Mapinduzi (CCM) lakini
walikosa maendeleo na baada ya kuchagua upinzani, hivi sasa Kigoma
imebadilika kwa kiasi kikubwa.
Alisema lazima wananchi wawe na upeo wa kufikiria kwani Mkoa wa Tabora
wenye majimbo tisa, hakuna hata moja ambalo limechukuliwa na upinzani na
matokeo yake hakuna maendeleo..Aliwataka
wananchi wa jimbo hilo kubadili uongozi uliopo kwani licha ya Mkoa huo
kubarikiwa Mawaziri, hadi leo hauna maendeleo ya kujivunia
No comments:
Post a Comment