Monday, 28 October 2013

CUF ni Saccos ya Seif - UVCCM

JUMUIYA ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) imesema  Chama cha Wananchi (CUF) ni  Chama cha Akiba na Mikopo (Saccos) kutokana na kauli iliyotolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif  Hamad kuwa ataendelea kuwania nafasi hiyo na kutangaza nia ya kuwania tena urais mwaka 2015.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Sadif Khamis Juma katika mkutano wa hadhara wa vijana wa CCM uliofanyika katika viunga vya Vuga.
Alisema kauli hiyo licha ya kwenda kinyume na misingi ya demokrasia, pia inaonyesha kiongozi huyo amejawa na  ubinafsi na tamaa ya kushika  madaraka.
Mwenyekiti huyo alisema uamuzi wa Maalim Seif wa kutangaza kuwa ataendelea kuchukua fomu ya kuwania ukatibu mkuu na urais wa Zanzibar mwaka 2015, si kwamba ni wa kidikteta, pia anaonyesha ni kiasi gani anavyokitumia chama hicho kama Saccos au kampuni yake binafsi.
“Kiongozi huyu ni hatari na hafai, anawatia hofu wanasiasa wenzake ili wasijitokeze kuwania nafasi hizo aendelee kujenga ngome ya utukufu wa kisiasa,” alisema huku akishangiliwa na wanachama wa CCM.
Pia aliponda kauli ya Maalim Seif kuwa ataendelea kuwania urais na hataacha siasa hadi atakapoishiwa nguvu au kukutwa na kifo, akisema maneno hayo ni aibu kwa kiongozi anayejifanya muumini wa misingi ya demokrasia.

No comments:

Post a Comment