Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) linakutana leo jini Dodoma huku hatma ya Mwenyekiti wa umoja huo, Sadifa Hamisi Juma ikiwa mashakani.
Mkutano huo wa baraza ulitanguliwa na kikao cha
Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM kilichokaa jana jioni mjini Dodoma kwenye
Ukumbi wa White House ambako ni makao makuu ya CCM.
Sadifa, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Donge,
analalamikiwa kutokana na matatizo mbalimbali ya kiutawala, matumizi
mabaya ya fedha na usimamizi mbovu wa mali za chama hicho.
Alipoulizwa juu ya kuwapo kwa vuguvugu la
kumng’oa, Sadifa alijibu kwa kifupi tu; “Asante Nashukuru.” “Ninaambiwa
nimekuwa mtu wa kutukana watu, nimemtukana nani? Asante
Nashukuru.,”aliongeza Sadifa hata pale mwandishi alipomuuliza kwa zaidi
ya mara tatu aliishia kutoa jibu: “Asante nashukuru.”
Naye Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda,
alipoulizwa na Mwananchi jana, alisema kuwa hana taarifa za kuwapo
mpango wa kumng’oa mwenyekiti wake kama inavyoelezwa.
“Sikiliza, mimi ndiye Mtendaji Mkuu wa UVCCM,
ajenda za mkutano, sisi kama sekretarieti tumeshaziandaa na hakuna
agenda kama hiyo. Umoja huu unaendeshwa kwa kanuni na taratibu,”alisema
Mapunda.
Mapunda aliyechukua mikoba hiyo Agosti mwaka huu,
alipoulizwa kuhusu mkutano huo kugharamiwa na CCM makao makuu badala ya
Jumuiya yenyewe, alikanusha taarifa zilizozagaa akisema: “Mimi ndiye
niliyeitisha mkutano huu, sasa chama kinatoka wapi?”
Mjumbe aanika madudu ya UVCCM
Mwenyekiti wa UVCCM wa Mkoa wa Ruvuma, Alex
Nchimbi alifafanua hakuna njama za kumtoa ila mambo anayotakiwa
kurekebisha ndio yanaweza kumtoa.
Nchimbi alisema kuwa UVCCM inakabiliwa na tatizo
la matumizi mabaya ya fedha na kibaya zaidi hesabu za chama hicho
hazijakaguliwa kwa muda mrefu.
Alisema jumuiiya hiyo hupata kiasi cha Sh80
milioni kutokana na miradi mbalimbali kama jengo lililoko makao makuu ya
UVCCM, lakini fedha hizo zinafujwa.
“Ila utashangaa kaka yaani zile fedha
zinavyofujwa. Hadi kwa mwezi jumuiya inabakiwa na Sh8 milioni au wakati
mwingine hadi Sh6milioni,” aliongeza Nchimbi.
Nchimbi aliongeza tatizo jingine ni uteuzi wa viongozi bila kufuata taratibu.
Alisema kuwa Sadifa aliteua sekretarieti kabla ya uteuzi wa wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ambapo ni kinyume na utaratibu.
Alitaja viongozi hao kuwa ni Mkuu wa Idara ya
Uchumi na Fedha, Omar Suleimani, Mkuu wa Chipukizi na Uhamasishaji, Omar
Justus na Tumaini Mwakasege, ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa
Oganaizesheni.
“Umoja wetu una pikipiki 10, lakini kapeleka
pikipiki mbili Morogoro na nane kazipeleka Zanzibar kwenye jimbo lake.
Ukichunguza uandikishaji wake utagundua bado zinamilikiwa na UVCCM”,
alisema Nchimbi.
Nchimbi pia alimtuhumu Sadifa kwa kuanzisha nafasi za makatibu wasaidizi wa mikoa bila ya baraka za Baraza Kuu.
“Hivi nani angewalipa watu hawa. Lazima tujiulize
UVCCM ina fedha gani za kuwalipa makatibu wa mikoa na wasaidizi?,”
alisema Nchimbi
Chanzo Mwananchi
Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment