Nguo hizo zimekuwa msaada mkubwa kwa Watanzania maskini, hasa wanawake kwani wakati mwingine huuzwa kuanzia Sh300 hadi Sh500.
Ni saa tano asubuhi jua linawaka, soko la Karume
wilayani Ilala jijini Dar es Salaam tayari limejaa watu wa kila rika.
Kwa jumla, ni mchanganyiko au mseto wa wafanyabiashara , wachuuzi na
hata wanunuzi.
Wengi waliomo ndani ya soko hilo kwa maana ya
wanawake na wanaume ama wananunua au kuuza nguo , viatu chakavu ambavyo
tayari vimevaliwa na watu wa nchi tajiri za magharibi. Nguo hizo ndizo
zimepewa jina maarufu la mitumba.
Miongoni mwa ‘mitumba’ hiyo, ni nguo za ndani,
sidiria na hata chupi za kike na kiume, ambazo zimesheheni katika meza
nyingi za wafanyabiashara huku nyingine zikiwa zimetundikwa.
Ununuzi huo wa nguo za mitumba ni jambo ambalo
hadi asilimia 90 ya Watanzania hasa wa kipato cha chini au kawaida
wamelifanya kaitka maisha yao.
Baadhi yao wamezaliwa na kukuta utamaduni huo, nao
wakauendeleza na kisha kuurithisha kwa watoto wao. Zipo sababu nyingi
za wengi katika jamii kuendelea kununua na hata kuvaa mitumba, zikiwamo
za kiuchumi, mazoea.
Hata hivyo, wataalamu wa afya wanaonya na kusema
kuwa nguo hizi za mitumba, hususan za ndani zina madhara mengi kwa
wanawake na wanaume wanaopenda kuzitumia.
Hivi karibuni, Shirika la Viwango Tanzania (TBS),
limepiga marufuku na kutoa kipindi cha mwisho kwa wafanyabiashara hao
wanaouza nguo za ndani za mitumba, kuacha kuuza bidhaa hizo.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kipindi cha mpito
kuisha, ambapo kwa sasa TBS wamechukua uamuzi wa kuzichoma moto nguo
hizo. Msemaji wa TBS, Rhoida Andusamile anasema hatua hiyo ni
utekelezaji wa matakwa ya agizo la sheria ya mwaka 2009 inayozuia
matumizi ya nguo za ndani zilizokwishatumika.
Profesa Malise Kaisi wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya
Tiba Shirikishi Muhimbili (Muhas) anasema, yapo madhara makubwa ya kuvaa
nguo za ndani za mitumba kutokana na unyeti wa maeneo yanapovaliwa nguo
hizo.
Anasema, walioketi juu ya hatari zaidi ni
wanawake ambao maumbile yao yapo wazi zaidi na ni rahisi kwa vijidudu
kuingia kwa urahisi pindi wanapokaribia vitu hatarishi. Kwa mfano,
anasema, nguo za ndani zilizovaliwa huenda zina vijidudu vya fangasi au
chawa wa sehemu za siri, mwanamke anapovaa hupata maambukizi hayo.
“Endapo watavaa nguo hizo bila kuzifua kwa usahihi
na kuzichemsha, kisha kuzipiga pasi, ni rahisi kupata maambukizi.
Lakini pia, si vyema kimaadili kuvaa nguo zilizokwishavaliwa na watu
wengine” anasema Prof Kaisi.
No comments:
Post a Comment