Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, amepinga uamuzi wa kusimamishwa kwa maelezo kuwa kikao kilichochukua uamuzi huo hakitambuliki kikatiba huku akikanusha tuhuma za kutumiwa na Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, kukisambaratisha chama hicho.
Akizungumza jana na gazeti hili, Mwigamba alisema
kikao ambacho kina mamlaka ya kumwajibisha ni Kamati Kuu baada ya
kupokea tuhuma na kumsikiliza.
“Baraza la uongozi la Kanda halina mamlaka ya
kunisimamisha uenyekiti, lakini kwa kuwa mimi bado ni mwanachama hai wa
Chadema na sitahama Chadema, nitakaa pembeni ili chama kifanye uchunguzi
wa tuhuma zangu nikiwa nje ya ofisi,” alisema Mwigamba.
Hata hivyo, alisema anakusudia kufafanua chanzo
cha mgogoro wake na baadhi ya viongozi leo, baada ya kukabidhiwa
kompyuta mpakato (laptop) na viongozi wa chama hicho ambao waliichukua
ili kuifanyia uchunguzi.
Akana kutumiwa na Zitto
Akizungumzia tuhuma za muda mrefu kuwa, amekuwa
akitumiwa na Zitto hasa kuelekea uchaguzi ndani ya chama hicho,
alisema wanaofikiri hivyo ni vipofu wa kisiasa.
“Hizi tuhuma kuwa natumiwa na Zitto nimekuwa
nikizisikia, lakini huo ni upofu, mimi si mtu wa kutumika nina elimu
yangu nzuri ya shahada ya kwanza ya utawala wa biashara, najua
ninachokifanya ni kwa masilahi ya chama,” alisema Mwigamba.
Alisema kama angekuwa mtu wa kutumiwa sasa,
angetumiwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ambaye ana uwezo
wa kifedha kuliko Zitto au Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa ambaye atakuwa
mgombea wa urais wa chama hicho na ana uwezekano wa kushinda.
Alisema kabla ya tuhuma za sasa kwamba anatumiwa
na Zitto, aliwahi kutuhumiwa pia na Zitto kuwa anatuhumiwa na Mbowe hasa
kutokana na misimamo yake na kauli zake katika vikao na maeneo
mbalimbali, lakini baadaye ilithibitika kuwa alikuwa na hoja za msingi.
“Mimi ni mwanachama hai wa Chadema na nimekuwa
nikitoa maoni yangu si kama Mwenyekiti wa Chadema Mkoa. Nina uhuru wa
kutoa maoni katika kuhakikisha chama changu kinashika dola,” alisema
Mwigamba.
Chanzo Mwananchi
Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment