Wakati Serikali ikiendelea kuikalia ripoti ya Tume ya Kuchunguza
Matokeo ya Kidato cha Nne iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
mapema mwaka huu, baadhi ya wajumbe wake wameanika madudu mengi
yaliyobainika katika uchunguzi huo.
Mmoja wa wajumbe waliounda Tume hiyo ameliambia
gazeti hili hivi karibuni kuwa waligundua mambo mengi yanayodhihirisha
udhaifu mkubwa katika uendeshaji wa sekta ya elimu nchini, ikiwa ni
pamoja na kubaini kuwa idadi kubwa ya wakuu wa shule hawana elimu ya
shahada.
Alieleza kuwa kiutaratibu mkuu wa shule anatakiwa
kuwa na elimu isiyopungua shahada pamoja na mafunzo ya uongozi na
usimamizi. “Kumbukumbu zilionyesha kuwa elimu ya sekondari ya kawaida
ina jumla ya shule 4,528. Wakuu wa shule 1,498 wana shahada ya kwanza au
zaidi, 1,703 wana stashahada, 33 wana sifa nyingine” alisema.
Sehemu kubwa ya matokeo ya uchunguzi huo
inasemekana yamejikita zaidi katika kuzitupia lawama taasisi za Baraza
la Mitihani la Taifa (Necta) na Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE).
Udhaifu wa kiutendaji kati ya taasisi hizo mbili
unadaiwa umechangia kwa wanafunzi wengi kufanya vibaya kwenye mitihani
ya kidato cha nne mwaka jana, kiasi cha kuilazimisha Serikali kuunda
tume kuchunguza tatizo kutokana na kilio kikubwa cha wadau wa elimu na
wananchi.
Matokeo hayo ya mtihani wa kidato cha nne
uliofanyika mwaka jana yanaonyesha kuwa watahiniwa 240,903 sawa na
asilimia 60.6 walipata sifuri, huku wanafunzi 23,520 tu ambao ni sawa na
asilimia 5.16 ndiyo waliofaulu na wengine 103,327 sawa na asilimia
26.02 wakiwa wamepata daraja la nne.
Katika mtihani huo, watahiniwa 397,136 walikuwa wa shuleni na 68,806 wa kujitegemea.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu Pinda aliamua
kuunda Tume iliyoanza kufanya kazi kuanzia Machi hadi Juni mwaka huu.
Tume hiyo iliyokuwa inaongozwa na Profesa Sifuni Mchome ilimkabidhi
Waziri Mkuu ripoti Juni 15, mwaka huu.
Hata hivyo, ripoti hiyo haijawahi kutolewa
hadharani baada ya Tume kumaliza kazi yake, huku Profesa Mchome ambaye
alikuwa Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Vyuo Vikuu Tanzania akipandishwa
cheo na kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
No comments:
Post a Comment