Friday, 25 October 2013

Seif bado ataka urais • Asema haachi hadi afukuzwe na wananchi

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Seif Sharif Hamad, ametangaza azima yake ya kuendelea kugombea urais visiwani humo pamoja na ukatibu mkuu wa Chama chake cha Wananchi (CUF).
Hamad alitangaza msimamo huo jana alipokuwa akizungumzia miaka mitatu ya utendaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Awamu ya Saba, katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Zanzibar Ocean View.
Alisema kuwa atastaafu siasa pale atakapoishiwa nguvu mwilini, kwamba licha ya watu kumuona kuwa ni kizingiti kwa matakwa yao, hataacha nia yake hiyo ya kuongoza Wazanzibari.
“Hamuwezi kwa matakwa yenu kuona Seif ni kizingiti niondoke, siondoki! Mimi nitaendelea kuwatumikia Wazanzibari ndio ahadi yangu niliyotoa labda nipate maradhi au niishiwe nguvu,” alisema Hamad baada ya kuulizwa swali kuwa anafananishwa na Robert Mugabe wa Zimbamwe kwa kung’ang’ania madaraka.
Kuhusu kugombea tena nafasi yake ya ukatibu mkuu katika uchaguzi wa CUF utakaofanyika mwakani na urais wa Zanzibar mwaka 2015, Seif alisema kuwa atatoka tu endapo wanachama watakapofanya uamuzi wa kutomchagua.
Alisema uchaguzi wa CUF katika matawi yote nchini utafanyika mwezi ujao, Mei na Juni mwakani watakuwa na mkutano mkuu wa taifa wa CUF.
Hamad alianza kugombea urais wa Zanzibar kwa mara ya kwanza mwaka1995 baada mfumo wa vyama vya vingi kurejeshwa rasmi lakini alishindwa, akafanya hivyo tena mwaka 2000, 2005 na 2010 nako akapigwa mweleka na CCM.
Katika hatua nyingine, Seif alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa busara zake za kuona kuna umuhimu wa kuandika Katiba mpya.
“Mimi nampongeza Rais Kikwete katika suala hili. Yeye alisema wazi kwamba baada ya miaka 50 lazima tuwe na katiba ambayo inakidhi mahitaji ya wakati huu.
“Katiba ambayo angalau itachukua miaka 50 mingine. La msingi zaidi ni kwamba wananchi washirikishwe kikamilifu,” alisema.
Alisisitiza kuwa uamuzi aliochukua Rais Kikwete ni mzuri japo una changamoto zake, hivyo hatua inayoendelea hivi sasa ni Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuendelea kuchambua maoni ya mabaraza hayo, hatimaye iweze kupatikana rasimu ya pili ambayo ndiyo itakayopelekwa kwa rais, ambayo ataiwasilisha kwa Bunge Maalumu la Katiba.
Alisema kuwa azima njema ya kuifanya nchi iwe na Katiba mpya ifikapo mwakani, lazima kukiri kuwa kuna changamoto nyingi zinazoendelea kujitokeza katika suala hilo.
Alisema baada ya vurugu mbalimbali kujitokeza kuhusu mchakato huo wa Katiba, Rais Kikwete aliona busara ya kukaa meza moja na viongozi wa vyama vyote vya siasa vilivyosajiliwa ili kuyajadili kwa upeo wake mambo yanayolalamikiwa.
Seif alisema matarajio yake ni kwamba vikao vilivyofanyika na maazimio yake kati ya Rais Kikwete na viongozi wa vyama vya siasa yataweza kuzaa maafikiano mema.
Awali akieleza mafanikio yaliyofanywa na serikali ya umoja wa kitaifa, alisema wamepandisha bei ya karafuu, hali iliyowapa wakulima ahueni kubwa ikilinganishwa na ilivyokuwa huko nyuma.
“Hadi juzi jumla ya tani 1,540 tayari zimenunuliwa kwa kiasi cha sh bilioni 21.5,” alisema na kuongeza kuwa kupandishwa kwa bei ya karafuu kumewafanya wananchi wengi hasa katika vijiji vya Pemba kujenga nyumba bora zaidi.
Mafanikio mengine ni kuongeza masilahi ya wafanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi katika mwaka 2010/2011 mishahara ya wafanyakazi wa serikali iliongezwa.
“Katika mwaka 2011/2012 serikali ilishughulika na suala la kupanga skimu kwa wafanyakazi wa wizara na taasisi za serikali ili kila mmoja ajijue yuko wapi, lengo likiwa ni kupandisha mishahara tena katika mwaka huu wa fedha 2013/2014,” alisema.
Chanzo Tanzania Daima.

No comments:

Post a Comment