KIRAKA na mchezaji anayetumia nguvu nyingi wa Yanga, Mbuyu Twite ametoa ya moyoni.
Mchezaji huyo raia wa Rwanda ameliambia benchi la
ufundi kwamba anacheza vizuri zaidi akisimama katikati na si pembeni
anakochezeshwa sasa.
Katika mechi ya Yanga iliyopita dhidi ya Rhino ya
Tabora, Twite alisimama kwenye nafasi ya beki wa kati na Kelvin Yondani
baada ya Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kutokuwepo na sasa amesisitiza kuwa
anajisikia raha zaidi akiendelea kusimama hapo.
Twite amekuwa akichezeshwa nafasi ya beki wa kulia
wa Yanga ingawa ana uwezo wa kucheza pia kushoto na kwenye kiungo akiwa
na maana kwamba anataka kucheza katikati ama kwenye nafasi ya Yondani
au ya Cannavaro.
“Katika namba zote, nafurahia zaidi ninapocheza
beki wa kati namba nne na tano, ni nafasi ninayoipenda kuliko nyingine
zote na kiukweli ninapopangwa hapo huwa naifurahia kucheza.”
“Lakini pamoja mapenzi yangu, huwa sichagui nafasi
ya kucheza, mahali popote ambako kocha atanipanga niko tayari iwe
kulia, kushoto, kiungo kokote sawa, anayejua anajua tu, lakini
ningefanya kazi vizuri zaidi pale katikati,”alisema Twite na kuongeza
kwamba yeyote atakayepangwa naye kwenye ulinzi atapiga naye kazi wala
habagui kwavile amefanya nao mazoezi na anawajua.
Tangu ametua Yanga msimu uliopita, amekuwa beki wa
kulia wa kudumu ingawa mara nyingine kunapotokea mapungufu kwenye
nafasi ya beki wa kati inayochezwa na Cannavaro na Kelvin Yondani au
kiungo mkabaji.
Twite ndiye aliyeanza kumuweka benchi nahodha wa
Yanga aliyetemwa, Shadrack Nsajigwa. Benchi la ufundi lilimpa kipaumbele
Twite kwavile ana uwezo wa kucheza namba zaidi ya moja na kusaidia timu
kwa lolote linaloweza kutokea ndani ya dakika 90.
No comments:
Post a Comment