Katika mahojiano maalumu na timu ya waandishi wa Mwananchi na
The Citizen jana, Graf alisema kuwa Serikali ya Tanzania inapaswa
kusaini mkataba wa kimataifa wa kubadilishana taarifa za masuala ya
usimamizi wa fedha na kodi ili kuweza kujua ni kina nani wameweka fedha
nchini kwake na kunufaika na kodi.
Graf, ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi
nchini, alisema kuwa hivi karibuni Serikali ya Uswisi ilisaini mkataba
wa kimataifa wa kubadilishana taarifa kuhusu masuala ya fedha, ambao
unajulikana kwa lugha ya Kiingereza kama `Convention on Mutual
Administrative Assistance in Tax Matters’.
Alisema ikisaini mkataba huo ina maana itasaidiwa na Serikali ya Uswisi kupata fedha zilizofichwa na Watanzania.
“Serikali ya Tanzania inatakiwa kuweka mkakati wa
kisheria utakaotengeneza mazingira ya kubadilishana taarifa za fedha na
mataifa mengine. Kwa jambo hilo hata Serikali ya Uswisi inaweza kusaidia
katika kupatikana kwa fedha zilizofichwa,” alisema Graf, ambaye
anaongoza Serikali ya Uswisi kwani kwa kawaida Rais wa Bunge ndiye pia
kiongozi wa taifa hilo.
Graf alisema kwa sasa itakuwa ngumu kwa Tanzania
kupata fedha hizo kwani haijasaini mkataba wa kimataifa wa kubadilishana
taarifa za fedha na mataifa mengine.
Alieleza pia katika miaka ya karibuni Serikali ya
Uswisi imeandaa muswada wa sheria wa kubana fedha zilizopatikana kwa
njia za kifisadi na kufichwa katika benki za Uswisi. Graf alisema sheria
hiyo ikipita itaruhusu Serikali ya nchi hiyo kutaifisha fedha ambazo
zimepatikana kwa njia haramu na kufichwa katika benki za huko.
Muswada huo unaoitwa kwa lugha ya Kiingereza
`Freezing and Restitution of Assets of Politically Exposed Persons
obtained by Unlawful Means Bill’ ulisomwa kwa mara ya kwanza kwenye
Bunge la nchi hiyo mwezi Mei, mwaka huu.
Graf alisema faida nyingine ya Tanzania kusaini mkataba huo ni kuwa, itaweza kuwatoza kodi Watanzania hao walioweka fedha huko.
Alifafanua kuwa siyo fedha zote zinazowekwa kwenye
benki za Uswisi kuwa ni haramu kwani kuna nyingine zimepatikana
kihalali, lakini zinaweza kutozwa kodi.
“Tanzania inakosa kodi kutokana na fedha
zilizohifadhiwa na Watanzania wenye akaunti kwenye benki za Uswisi,”
aliongeza Graf, ambaye alichaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo Novemba 26,
2012 na kutakiwa kukaa madarakani kwa mwaka mmoja.
Graf alisema pia fedha za kodi zingeisaidia Tanzania kugharimia sekta mbalimbali za maendeleo.
Chanzo Mwananchi
Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment