Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, ameonya viongozi na watendaji wa CCM nchini kutowapitisha wagombea wasio waadilifu katika chaguzi zijazo kwa sababu itapunguza idadi ya kura huku akiwasisitiza kuliangalia matakwa ya kundi kubwa la wapigakura ambalo ni vijana.
Makamba ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya
Taifa ya chama hicho, aliyasema hayo jana wakati akiwasilisha mada
katika mafunzo ya viongozi na watendaji wa CCM nchini (makatibu wa
wilaya na mkoa).
Kwa mujibu wa chanzo kutoka ndani ya kikao hicho
kilisema “Makamba alisema pamoja na kutekeleza Ilani ya uchaguzi kwa
asilimia 100 ama kuwa na ilani nzuri ya uchaguzi bila kuwa na mgombea
mwadilifu chama chetu hakitaweza kufanya vizuri katika chaguzi hizo
zijazo.”
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Makamba alisemam,
wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho 2005, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa
aliwahi kuwaambia wajumbe pamoja na kuangalia ndani ya chama waangalie
na nje ya chama wakati wanamchagua mgombea urais.
Imedaiwa kuwa mbunge huyo pia aliwataka viongozi
na watendaji wa CCM, kuhakikisha wanasimama upande wa wananchi badala ya
watu wachache.
Kuhusiana na makundi ndani ya chama hicho, Makamba
alisema makundi hayakuanza wakati wa mfumo wa vyama vingi bali
yalikuwapo hata wakati wa chama kimoja.Alisema makundi yaliyopo hivi
sasa ni hatari kwa chama kwa sababu ni ya kumbeba mtu na yanaendelea
kuwapo hata baada ya uchaguzi.
Chanzo hicho kimesema, Makamba ameshauri
kufumuliwa kwa Sekretarieti ya Ajira ya Tamisemi na kuingizwa watendaji
wenye machungu na chama. Pia alitaka ajira ndani ya chama hicho zianzie
kwa watu wenye elimu ya shahada moja na kuendelea.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula,
katika mada yake inayohusiana na maadili, aliwaambia viongozi hao kuwa
hatakuwa na huruma na watendaji watakaobainika kuwasaidia wagombea wasio
waadilifu kupita katika kura za maoni.
No comments:
Post a Comment