Mwenyekiti Sadifa acheza sakakasi kukwepa kung’olewa, amteua hasimu wake kisiasa, Makonda na wengine watatu kuongoza
Dodoma. Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana alilazimika kuzima mapinduzi yaliyokuwa yamepangwa
kuwang’oa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana ya chama hicho (UVCCM), Sadifa
Juma Khamis na makamu wake, Mboni Muhita.
Jana Kinana akifungua mkutano wa Baraza Kuu la
jumuiya hiyo, aliweka bayana kuwa mkutano huo haukuwa kwa ajili ya
“kuibomoa UVCCM, bali kuijenga”, kauli ambayo inatajwa kuwa iliwavunja
nguvu wajumbe waliokuwa wamepanga kuanzisha harakati za kuwatoa
madarakani viongozi hao.
Habari zaidi kutoka Dodoma zilisema kauli ya
Kinana iliongeza nguvu harakati za kujinasua za Sadifa ambaye usiku wa
kuamkia jana, alikesha akifanya vikao vya kuwaomba radhi wenyeviti wa
UVCCM wa mikoa na baadaye wajumbe wote wa Baraza Kuu.
“Hatua hiyo nadhani imemsaidia sana maana wenzake
ndani ya umoja huo hawaridhiki na jinsi mambo yanavyokwenda, pamoja na
uongozi wake. Wanaona kama hakidhi standards (viwango) zao,” kilisema
chanzo chetu kutoka ndani ya mkutano huo.
Hii ni mara ya pili kwa Katibu Mkuu huyo kumwokoa
Sadifa, kwani Septemba mwaka huu, alilazimika kuingilia kati mgogoro
ambao uliibuka katika kikao cha Baraza Kuu la jumuiya hiyo Visiwani
Zanzibar baada ya wajumbe kutaka kumwajibisha kwa madai kwamba alikiuka
kanuni za uteuzi wa wakuu wa idara za UVCCM.
Pamoja na kauli elekezi ya Kinana, Sadifa ambaye
pia ni Mbunge wa Donge, Zanzibar alilazimika kucheza sarakasi
zilizomwezesha kuzima mapinduzi yaliyokuwa yameandaliwa dhidi yake.
Mwenyekiti huyo aliongoza kikao cha Baraza Kuu kwa saa tatu na
kukamilisha ajenda zilizokuwa zimepangwa, ikiwa ni pamoja na
kuwaidhinisha wakuu wapya wa idara za jumuiya hiyo, kisha aliahirisha
mkutano huo mara tu baada ya kuibuliwa kwa hoja ya kutaka kumjadili.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana jioni
zilisema, Mwenyekiti wa UVCCM, Mkoa wa Mbeya, Amani Kajuna ndiye
aliyeibua hoja ya kutaka Sadifa ajadiliwe kutokana na kile alichosema
kuwa kiongozi huyo ameifanya jumuiya hiyo kushindwa kutekeleza wajibu
wake ipasavyo.
“Kama tunataka kusonga mbele katika jumuiya yetu,
lazima tuhakikishe kwamba tunaisafisha nyumba yetu ili tukitoka hapa
wote tuwe tunazungumza lugha moja. Kwa hiyo napendekeza mwenyekiti atoke
nje ili tumjadili,” chanzo chetu kilimnukuu Kajuna.
Habari zaidi zilidai mapendekezo hayo ni kama
yaliungwa mkono na baadhi ya wajumbe, akiwamo Mwenyekiti wa UVCCM wa
Mkoa wa Dodoma, Henry Msunga ambaye alisimama na kusema: “Hiyo ni hoja
ya msingi sana”.
Hata hivyo, wakati wajumbe wengine wengi wakiwa
wameinua mikono yao juu wakitaka kuchangia pendekezo hilo, Sadifa
alisimama na kuanza kuzungumza huku akiomba msamaha kwa upungufu wa
kiuongozi unaojitokeza na katika hali isiyotarajiwa aliahirisha rasmi
mkutano huo.
Kajuna na Msunga kwa nyakati tofauti jana,
walilithibitishia gazeti hili kuwapo kwa matukio hayo, lakini walikataa
kuyazungumzia kwa undani huku wakisema kuwa bado wana fursa katika vikao
vijavyo kwa ajili ya kurekebisha mambo ndani ya jumuiya hiyo.
“Mimi bado nina imani na jumuiya yetu, maana watendaji ambao
tumewapitisha leo (jana) ninaamini watafanya kazi nzuri. Sisi viongozi
wa mikoa tuko vizuri na tuna wanachama wengi, kwa hiyo jumuiya
itaendelea kuwa imara,” alisema Kajuna.
Kwa upande wake, Msunga alisema: “Baada ya hoja
kuibuliwa kweli mimi niliiona ni ya msingi sana, ila nimeridhika na
maelezo kwamba mkutano ulikuwa na ajenda maalumu kwa hiyo ninachoamini
ni kwamba fursa bado ipo, tutakapokutana tena tutakuwa na nafasi ya
kurekebisha kasoro zinazojitokeza”.
Jitihada za kumtafuta Sadifa hazikufanikiwa jana,
baada ya gazeti hili kuambiwa kuwa alikuwa kwenye kikao cha Kamati ya
Utekelezaji ya jumuiya hiyo, kilichokutana jana usiku.
Chimbuko la mapinduzi
Mpango huo wa mapinduzi ulikuwa ni mwendelezo wa
fukuto lililoanzia katika Mkutano Maalumu wa Baraza Kuu lililofanyika
Zanzibar mapema Septemba mwaka huu, wakati wajumbe walipowakataa wakuu
wa idara za UVCCM kwamba hawakuwa halali kutokana na uteuzi wao
kutofuata taratibu na kanuni za jumuiya hiyo.
Mapema jana kabla ya kuzuka kwa hoja za kutaka
kumjadili Sadifa, baraza hilo liliwapitisha wakuu wa idara wapya watatu
akiwamo hasimu wa kisiasa wa mwenyekiti huyo wa UVCCM, Paul Makonda
ambaye sasa ataongoza Idara ya Chipukizi na Uhamasishaji.
Makonda mara baada ya kushindwa katika Uchaguzi
Mkuu wa jumuiya hiyo mwishoni mwa mwaka jana alipokuwa akiwania nafasi
ya makamu mwenyekiti, aliteuliwa kuwa mjumbe wa Baraza Kuu lakini
aliikataa nafasi hiyo.
Hatua hiyo ilimgharimu katika kikao cha Baraza Kuu
la UVCCM, Februari mwaka huu, wakati alipokwenda Dodoma kwa mwaliko wa
kuhudhuria kikao hicho, lakini baada ya kuchukua posho, alitimuliwa kwa
maelezo kwamba aliwahi kukataa nafasi hiyo.
Taarifa ambazo gazeti hili lilizipata na
kuthibitishwa na Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda zilisema wengine
walioteuliwa na kuidhinishwa na Kikao cha Baraza Kuu ni Zainabu Katimba
atakayeongoza Idara ya Oganaizesheni na Omari Suleiman ambaye amepewa
Idara ya Fedha na Uchumi.
Sadifa ambaye pia ni Mbunge wa Donge aliwahi
kulalamika juu ya kuwapo kwa kundi la vijana ambao wamekuwa wakimpiga
vita sambamba na kuingilia utendaji wa kazi zake za kila siku kinyume
cha katiba ya jumuiya hiyo.
Chanzo MWANANCHI
Chanzo MWANANCHI
No comments:
Post a Comment