Monday, 21 October 2013

Suarez, Sturridge katika ushirikiano wa mashaka ndani ya Liverpool


LIVERPOOL kwa sasa ni kali, mtu akibisha anakuwa jeuri tu.Inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu England ikiwa na pointi 16 baada ya kucheza mechi saba unawezaje kusema siyo wakali?
Hata hivyo ukali wa kikosi hicho kwa sasa umechangiwa na juhudi kubwa na ushirikiano kati ya mastraika Daniel Sturridge na Luis Suarez.
Ushirikiano wa wachezaji hao msimu huu umewashangaza wapenzi wengi wa soka. Mbio, maarifa, kumiliki mpira kwa muda mrefu na kutikisa vyavu ni baadhi ya sifa za wachezaji hao msimu huu.
Kiwango chao kimefanya wafunge jumla ya mabao 11 mpaka sasa. Wachezaji hao wamepewa jina la pamoja la S.A.S, hapo mashabiki wanakumbuka wachananyavu wa siku za nyuma wa  Blackburn Rovers, Alan Shearer na Chris Sutton.
Kwa sasa mashabiki wanashangilia, angalau wamefutwa machozi ambayo yamekuwa yakiwatoka kwa misimu kadhaa. Lakini, mashabiki wa klabu hiyo watacheka kwa muda mrefu? Jibu ni hapana, kwa sababu ushirikiano wa wachezaji hao unaweza kuvunjika wakati wowote.
Hebu tuone sababu za Liverpool kutokushangilia sana ikiwa na wakali hao waliopachikwa jina ka S.A.S.
Suarez mguu ndani nje
Liverpool wamefurahia juhudi za klabu kumbakiza Suarez, wakati mchezaji huyo alipotaka kuondoka, lakini wafahamu kuwa lengo la nyota huyo wa Uruguay lipo palepale, anasubiri dirisha lingine la usajili ili aanzishe sokomoko jipya.
Mchezaji huyo amesema kocha wake hamwamini sana na haoni sababu ya kuendelea kucheza ligi ambayo vyombo vya habari vinammulika yeye tu uwanjani.
Mchezaji huyo aliwahi kuongeza kuwa anataka kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya na si vinginevyo. Lakini nani anaweza kumlaumu. Suarez kwa sasa ana umri wa miaka 26 na muda wa kucheza umeanza kumtupa mkono taratibu, anahitaji kutimiza malengo yake.
Suarez alishawahi kusema  hawezi kukataa kuhamia kwenye klabu kubwa kama Real Madrid au Bayern Munich. Kipaji cha Suarez kinatosha kupata ubingwa wowote, lakini akiwa na Liverpool, nafasi yake inakuwa finyu.
Mashabiki wa Liverpool wanashangilia na kutoa jina la  S.A.S kwa Sturridge na Suarez, lakini ukweli unabaki palepale kuwa ni vigumu kwa wachezaji hao kufikia kiwango cha wachezaji wenye jina halisi. 
Wakati Chris Sutton na Alan Shearer walipokuwa wakitamba, walifunga jumla ya mabao 96 katika kipindi cha msimu miwili tu. Suarez na Sturridge wana kiwango lakini ni mapema mno kuanza kuwapa majina ya wakongwe waliotikisa.
 Uwezekano wa kuumia
Suarez na Sturridge wanategemewa sana hasa baada ya kufunga mabao 11 kwa pamoja msimu huu, lakini nani anaweza kutabiri ya kesho? Mmoja wa wachezaji  hao akiumia ni wazi kuwa timu itatetereka.
Mwisho mwa msimu uliopita, Sturridge aliandamwa na majeruhi, nani ajuae kwamba atadumu kwa muda mrefu msimu huu. Licha ya maumivu, mchezaji kama Suarez, anaweza kukosekana uwanjani kutokana na ukorofi wake. Amerudi uwanjani hivi karibuni baada ya kumaliza adhabu ya kufungiwa mechi 10 kwa kumng’ata beki wa Chelsea, Branislav Ivanovic msimu uliopita na katika msimu wa  2012/2013 pekee alipata kadi 10 za njano.
Jina la mchezaji huyo si geni kwenye vitabu vya kumbukumbu za marefa na anaweza kuadhibiwa wakati wowote.
Watachoka kutegemewa
Unaweza kuona kituko kwa timu kusubiri wachezaji wawili tu, wapike mabao na kufunga. Kibaya ni kwamba, ni wachezaji wanne tu wa klabu hiyo ambao wamekutana na nyavu tangu msimu ulipoanza. Licha ya Suarez na Sturridge, wachezaji wengine waliokutana na nyavu ni Steven Gerrard na Victor Moses.
Kocha amekuwa na chaguo la wachezaji lisilobadilika na jambo hilo ndio limefanya Fabio Borini ajiunge na Sunderland kwa mkopo wa muda mrefu.
Mshambuliaji pekee aliyebaki kwenye akiba ya kocha Brendan Rodgers ni Aspas, ambaye kwa sasa hatishi sana. 
Kama wachezaji wanaopangwa mara kwa mara wakishindwa kufanya vizuri, itakuwa ni kazi kubwa kutabiri mabao.erpool yatatokea upande gani. Kocha Rodgers anahitaji ‘Plan B’ hasa katika kuwatengenezea mazingira ya kutamba, Suarez na Sturridge.

Mwanasipoti
 

No comments:

Post a Comment