Monday, 21 October 2013

Vigogo 21 vyatanguliza utamu Brazil 2014


Timu 32 ndizo zitakazoshiriki michuano hiyo, lakini hadi sasa ni 21 tu ndizo zilizofuzu. Kwenye Bara la Ulaya, tayari nchi tisa zimeshafuzu moja kwa moja na nne zinasubiri kucheza mchujo ili kupata idadi ya timu 13 zitakazofuzu kutoka barani humo.
Ubelgiji, Italia, Ujerumani, Uholanzi, Uswisi, Urusi, Bosnia, England na Hispania. Timu hizo zitaungana na timu nne nyingine zitakazopatikana baada ya mechi ya mchujo utakazohusisha timu za Croatia, Sweden, Romania, Iceland, Ureno, Ukraine, Ugiriki na Ufaransa.
Amerika Kusini; Brazil wamefuzu moja kwa moja kwa sababu ya kuwa wenyeji, wakati nchini nyingine kutoka bara hilo ni pamoja na Argentina, Colombia, Ecuador na Chile.  Kwenye orodha hiyo kuna timu moja hapo imekosekana ambayo itasubiri kucheza mchujo wa mechi itakayohusisha na bara lingine.
Ili kukamilisha idadi kamili ya timu zitakazofuzu kupitia bara hilo, Uruguay italazimika kucheza mechi na Jordan kutoka Bara la Asia ili kupata tiketi moja iliyobaki.
Kwa upande wa Amerika Kaskazini na Kati; Marekani, Costa Rica na Honduras zimefuzu moja kwa moja, wakati Mexico italazimika kucheza na New Zealand ili kufuzu, kinyume cha hilo, basi mastaa kama Javier Hernandez ‘Chicharito’ na Giovani Dos Santos watakuwa miongoni mwa wachezaji watakaokosekana.
Japan, Australia, Iran na Korea Kusini zenyewe muda mrefu tayari zilishafuzu fainali hizo, wakati Bara la Afrika hadi kufika mwishoni mwa Novemba timu tano zitakazowakilisha bara zitakuwa zimepatikana.

Miamba ya Afrika
Ghana inaonekana kama tayari imeshaweka mfukoni tiketi yake ya kutua Brazil mwakani baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya Misri kwenye mechi yake ya kwanza ya mchujo.
Ivory Coast nao walianza vizuri nyumbani kwa kuinyuka Senegal mabao 3-1, huku Nigeria ikishinda ugenini kwa Ethiopia mabao 2-1 na Burkina Faso waliibuka na ushindi mbele ya Algeria baada ya kushinda 3-2.
Mechi ambayo hadi sasa bado ngumu ni Cameroon na Tunisia, ambapo sare ya bila kufungana, inaipa nafasi Tunisia kama itafanikiwa kupata sare ya mabao ya aina yoyote mjini Yaounde, Cameroon mwezi ujao.
Burkina, Ivory Coast na Cameroon bado hazina uhakika sana licha ya matokeo yao ya mechi za kwanza kuwa mazuri, huku Nigeria ikiamini ushindi wao wa ugenini unawaweka kwenye nafasi nzuri pamoja na kocha wao, Steven Keshi kudai kwamba kazi bado haijakwisha mbele ya Ethiopia. Mechi za marudiano zitachezwa kati ya Novemba 16 na Novemba 19 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment