Friday, 25 October 2013

PAPA AMTIMUA ASIKOFU MPENDA RAHA


Kumekuwa na kelele za waumini nchini Ujerumani wakishinikiza askofu huyo afukuzwe kwa kukiuka taratibu.
Vatican City. Makao Makuu ya Kanisa Katoliki Duniani (Vatican) yamemsimamisha kazi Askofu wa Jimbo la Limburg, Ujerumani Franz-Peter Tebartz-van Elst anayekabiliwa na kashfa ya matumizi mabaya ya fedha kwa shughuli za kifahari.
Vatican ilieleza jana kuwa uamuzi huo umechukuliwa baada ya kuridhika kuwa Askofu van Elst amekiuka maadili yaliyowekwa na Papa Francis kwa viongozi walioko chini yake akiwataka waishi maisha ya uchaji, umaskini.
Hadi sasa, kumekuwa na kelele nyingi miongoni mwa waumini nchini Ujerumani wakitaka askofu huyo afukuzwe kazi.
Miongoni mwa matumizi yake makubwa ni ujenzi wa makazi yake binafsi yaliyogharimu Euro 2.9 milioni (Dola 3.9 milioni), ukumbi wa chakula wenye mita za mraba 63 ambao ni pamoja na mesi na bafu yenye thamani ya Euro 15,000.
Askofu van Elst (53) amekuwa akituhumiwa kuendesha miradi hiyo kwenye mji wa kihistoria wa Limburg, ikiwamo makumbusho, kumbi za mikutano, kanisa dogo na nyumba ya makazi yake binafsi.
Fedha hizo zinatokana na mapato ambayo ni misamaha ya kodi kwa vikundi vya kidini nchini Ujerumani kwa mujibu wa sheria.
“Baada ya uchunguzi wa awali, Vatican imeamua kuchukua hatua kumsimamisha na kumwondoa kwenye usimamizi wa jimbo,” ilieleza taarifa hiyo.
“Baba Mtakatifu (Francis) amekuwa akifuatilia kwa karibu mambo yote yanayoendelea katika Jimbo la Limbuerg,” iliongeza taarifa hiyo.
“Hali hiyo imefikia mahali ambako kiongozi huyu hawezi kuendelea kusimamia kazi zake za kitume kama askofu wa jimbo.”
Hata hivyo, taarifa hiyo haikueleza ni kwa muda gani Askofu van Elst amesimamishwa kazi, ila iliongeza kuwa itategemea na kukamilika kwa uchunguzi, tathmini ya hali ya fedha ya jimbo na mambo mengine.
Wiki iliyopita, Askofu van Elst alisafiri hadi mjini Rome, Italia kwa ndege ya shirika la gharama nafuu, Ryanair kujieleza mbele ya Papa Francis – kutokana na madai kuwa alisafiri mwaka jana kwa ndege ya daraja la kwanza kwenda India na pia kutumia vibaya fedha.

No comments:

Post a Comment