Monday, 28 October 2013

Eti mishahara ya wabunge ni midogo!

Wakati mjadala wa usiri wa mishahara ya Rais na Waziri Mkuu ukiibuka, sasa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anna Makinda naye ameibuka akidai kuwa mishahara ya wabunge ni midogo kiasi kwamba wabunge hao huwa na maisha magumu wanapostaafu.
Mjadala wa mishahara ya Rais na Waziri Mkuu uliibuka baada ya Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe kuitaja hadharani alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara wilayani Igunga Mkoa wa Tabora, hivi karibuni.
Zitto alisema Rais analipwa Sh384 milioni kwa mwaka sawa na wastani wa Sh32 milioni kwa mwezi bila kukatwa kodi, huku Waziri Mkuu akichukua Sh26 milioni kwa mwezi.
Hatua hiyo imepingwa na baadhi ya wanasiasa, akiwemo Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai akisema mshahara wa mtu ni siri yake, huku Waziri wa Nchi Katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumishi wa Umma, Celina Kombani akisema ni kinyume cha sheria.
Nacho Chama cha Watumishi wa Serikali Kuu na Afya (Tughe), kimekosoa hatua hiyo huku kikitaka Zitto ashitakiwe kwa kutaja hadharani mishahara hiyo.
Itoshe tu kusema kuwa, bado tuna safari ndefu ya kuikomboa nchi yetu katika lindi la umaskini.
Mishahara ya viongozi wakubwa kama hawa kwa nchi zilizoendelea iko wazi na wananchi wanaweza kuhoji. Kwetu ni siri kubwa, siri hii ya nini?
Kwa upande wake Spika Makinda akizungumza na Rais wa Bunge la Uswisi, Maya Graf aliyemtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam alisema, mishahara ya wabunge ni midogo kiasi kwamba wabunge hao huishi maisha magumu baada ya kustaafu.
Kutokana na hali hiyo, Makinda alisema wanaandaa mpango wa kuwaokoa wabunge wanapostaafu kwa kuwafundisha ujasiriamali.
Siyo kwamba napinga wabunge kuwa na maisha bora, lakini tulinganishe hiyo inayoitwa mishahara midogo na hali ya maisha yetu.
Hadi mwaka huu, wabunge wetu wanalipwa mshahara wa Sh11 milioni mbali na posho za Sh330,000 kwa siku ambazo ni sawa na Sh80,000 ya kujikimu akiwa nje ya jimbo, Sh200,000 ya kuhudhuria kikao kwa siku na mafuta ya gari ya Sh50,000.
Isitoshe, wabunge hupewa Sh30 milioni ya jimbo kwa mwaka. Halafu wakimaliza kipindi cha miaka mitano hulipwa kiinua mgongo cha Sh72 milioni.
Halafu Spika Makinda anasema eti mbunge akishakomba mamilioni hayo anakuwa na maisha magumu. Eti wabunge waliostaafu huenda ofisini kwake kumlilia hali ngumu ya maisha! Mimi hainiingii akilini hata kidogo.
Nasema hivyo kwa sababu, hiyo posho tu ya Sh330,000 wanayolipwa kwa siku imezidi kima cha chini cha mshahara wa wafanyakazi wa Serikali ambacho ni Sh150,000
Shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini (Tucta) limepambana kuhusu kima hicho cha mshahara walau kifikishwe hadi Sh350,000, lakini imeshindikana.
Walichoambulia kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete mwaka 2010 walipotishia kugoma ni vitisho na kejeli. Mshahara wa wafanyakazi wa umma haujapanda hadi leo kufikia kiwango hicho, badala yake zimebaki porojo tu.
Hicho kiinua mgongo (gratuity) cha Sh72 milioni kwa miaka mitano wanachochukua ni sawa na pensheni ya mtumishi wa umma, tena wa cheo cha juu akifanya kazi kwa miaka 40 hivi.
Hiyo Sh30 milioni wanayopewa kila mwaka kwa ajili ya mfuko wa jimbo, nani anaifuatilia? Kuna Mbunge anayekaa na wananchi wake jimboni kupiga hesabu imetumikaje?
Mbona kila siku wananchi wanaambiwa ahadi za uchaguzi zinatekelezwa na Bajeti ya Serikali na misaada ya wahisani?
Ama kweli aliyeshiba, hamjui mwenye njaa. Mtu anayelipwa mshahara wa mamilioni eti leo anaishi maisha ya shida, vipi yule asiye na ajira rasmi?
Kuna wananchi wangapi wanaoishi kwa kubangaiza maisha ya kuungaunga. Hawana uhakika hata wa kipato, achilia mbali hicho kiinua mgongo.
Fikiria kama asilimia 75 ya Watanzania wanategemea kilimo tena cha kujikimu. Wananchi hao wanategemea mvua inyeshe wapande na wavune ndipo wale na kuuza mazao yao. Mara uitasikia Serikali imekataza kuuza mazao yao nje ya nchi, ilimradi tu maisha yao hayana uhakika.
Ndiyo maana vijana wengi wamejazana mijini wakiuza pipi, nyembe maji, juisi na matunda barabarani. Wasipofanya hivyo, wakaishi wapi? Hawana ofisi ya kwenda kulia hali kama walivyo wabunge wastaafu.
Halafu unasikia wabunge wanavyobembelezwa kwa posho na mafunzo ya ujasiriamali. Huu ni kebehi kwa Watanzania.

No comments:

Post a Comment