HATIMAYE kitendawili cha uchaguzi mkuu wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) kimeteguliwa baada ya Jamal Malinzi kuibuka kidedea katika uchaguzi huo.
Malinzi aliibuka kidedea kwa kura 73 akimbwaga mpinzani wake pekee, Athuman Nyamlani (pichani) aliyepata kura 52.
Uchaguzi huo ulifanyika kwenye Ukumbi wa
Waterfront, Dar es Salaam ukitanguliwa na mkutano mkuu wa TFF
ulimalizika usiku wa kuamkia leo, Jumatatu saa saba na nusu.
Kuanzia asubuhi ya jana, Jumapili wapambe wa
wagombea hao wawili walijazana katika ukumbi huo, huku kila upande
ukijipa matumaini ya kukibeba kiti hicho.
Hata hivyo pengine kwa kusoma alama, Nyamlani
aliondoka ukumbini mapema kabla hata zoezi la kuhesabu kura halijaanza
hali ambayo tayari ilitoa dalili kwamba huenda mambo yalimuendea kombo.
Wakati Nyamlani akiondoka katika eneo la uchaguzi,
baadhi ya wapambe wa kambi ya Malinzi walianza kuzungumza katika
vikundi wakitambia ushindi wa mgombea wao.
Malinzi anatarajia kukabidhiwa rasmi ofisi na rais anayemaliza muda wake, Leodegar Tenga, Jumamosi ijayo.
Katika kinyang’anyiro cha Makamu Rais, Walace Karia
aliibuka kidedea kwa kuzoa kura 67 akiwabwaga
wapinzani wake, Ramadhan Nassib aliyepata kura 52 na Imani Madega
aliyeambulia kura sita.
Kufanyika kwa uchaguzi huo kunamaliza fitina za
wiki kadhaa zilizotawala medani ya soka nchini hususan katika nafasi ya
mwenyekiti ambayo ndiyo iliyokuwa na mvuto wa kipekee miongoni mwa wadau
wa soka nchini.
Uchaguzi huo unakuwa umeingiza sura mpya ambazo zitaliongoza shirikisho hilo kwa kipindi cha miaka minne ijayo.
Vipaumbele vya Malinzi alivyovinadi katika kampeni zake ni
pamoja na kukuza vipaji, kuboresha viwanja kwa kuanzisha kampuni tanzu
itakayoingia mkataba na wamiliki wa viwanja ambao ni Halmashauri
mbalimbali nchini na Chama cha Mapinduzi, kuwaendeleza waamuzi na
makocha kimafunzo ndani na nje ya nchi.
“Nikifanikiwa nitaanza kwa kupitia mikataba yote
ya wafanyakazi ukianza wa Katibu Mkuu, naamini wafanyakazi wote TFF wana
mikataba, nitaangalia namna ya kuwaboreshea mishahara na kuwapa
motisha, na nitaipitia mikataba ya wadhamini, kuna kampuni zinatangazwa
kuanzia ngazi za wilaya kuwa ni wadhamini lakini wilaya hazinufaiki.
“Vipengele tata vinavyokandamiza klabu katika
mikataba inayosimamiwa na TFF vitarekebishwa au kuondolewa kwa maslahi
ya soka na haki za klabu katika matangazo ya biashara zitalindwa kwa
nguvu zote,”alisema.
Malinzi (53) alizaliwa Agosti 8, 1960 mkoani
Kagera na kupata elimu yake ya sekondari mwaka 1974 hadi 1977 Mwanza
Sekondari na baadaye kujiunga na kidato cha tano na sita mwaka 1978 hadi
1981 Ilboru Sekondari.
Tangu mwaka 1999 amekuwa akijihusisha na masuala
mbali mbali ya michezo ikiwemo soka na ngumi.Ni dhahiri kwamba wadau
wengi wa soka watakuwa wakisubiri kwa hamu kuona Malinzi akitekeleza
ahadi hizo.
Sambamba na ahadi hizo, kuna kiu ya muda mrefu ya
mashabiki wa soka kutaka kuona timu yao ya taifa ikishiriki fainali za
Kombe la Mataifa ya Afrika na zile za Kombe la Dunia..
No comments:
Post a Comment