Chama cha Chadema kimeonya kuwa moto utawaka kwenye kikao cha Bunge kinachoanza wiki ijayo, iwapo wabunge wa CCM wenye msimamo wa kihafidhina watakwamisha marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iliyozua tafrani Bunge lililopita.
Akifungua mkutano wa baraza la uongozi la Chadema
Kanda ya Kaskazini jijini Arusha jana, Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema,
Freeman Mbowe alisema wabunge wa Chadema wanakwenda Dodoma wakiwa
wamejiandaa kupigania marekebisho ya sheria hiyo.
“Katika hili tutashirikiana na wabunge wote wa
vyama vyote wenye mapenzi mema wakiwemo wale wa CCM,ili kuhakikisha
Taifa linapata katiba bora” alisema Mbowe.
Alisema msimamo wa kupigania mabadiliko hayo
bungeni unachagizwa na makubaliano yaliyofikiwa wakati wa mazungumzo
kati ya vyama vya siasa na Rais Jakaya Kikwete, lakini akaonya kuwa
hawatasita kuhamishia mapambano hayo nje ya bunge kwa kushtaki kwa umma
iwapo hoja zao za msingi zitapuuzwa.
Rais Kikwete asikubali kutishiwa
Akizungumzia taarifa za kuwepo mkakati wa
kukwamisha marekebisho hayo miongoni mwa baadhi ya wabunge wa CCM, Mbowe
alimshauri Rais Jakaya Kikwete kutokubali kutishiwa na wabunge wachache
wanaoogopa mabadiliko.
“Wabunge wachache wanaotishia kukwamisha
marekebisho hayo hawako tayari kushuhudia Rais Kikwete akilivunja bunge
kwa sasa kama katiba inavyoelekeza, sababu wanaogopa uchaguzi kutokana
na kutokuwa na uhakika wa kurejea bungeni,” alisema Mbowe
Alishauri marekebisho ya sheria hiyo iliyotiwa
saini na Rais Kikwete Oktoba 10, mwaka huu lisiwe suala la majadiliano
bali yawe ni maagizo na maelekezo kutoka kwa Rais ambaye anapaswa
kutumia madaraka yake ya kikatiba kutimza lengo lake jema.
“Nashangazwa Rais Kikwete kukubali kutishiwa hata
na baadhi ya mawaziri aliowateua yeye, katika jambo hili jema la
kulipatia taifa katiba bora inayobeba maslahi ya Taifa kwa kuunganisha
Watanzania wote bila kujali itikadi zao kisiasa wala makundi yao
kijamii,” alisema Mbowe.
Chanzo Mwananchi
Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment