Hukumu ya muimbaji Nguza Viking aka Babu Seya na mwanaye Johnson Nguza aka Papii Kocha imepangwa kupitiwa tena October 30 mwaka huu na majaji watatu wa Mahakama ya rufaa nchini.
Babu Seya na Papii Kocha wanaendelea kutumikia kifungo cha maisha jela, baada ya kukutwa na hatia kwa makosa ya kubaka na kulawiti watoto wadogo. Hukumu hiyo ilitolewa Februari, mwaka 2010 na Jopo la majaji wakiongozwa na Natharia Kimaro.
Watoto wawili wa Babu Seya, Nguza Mbangu na Francis Nguza waliachiwa baada ya kubainika hawana hatia kwa makosa ya kubaka na kulawiti watoto. Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya Mahakama ya Rufani, mapitio ya hukumu hiyo yatasikilizwa Oktoba 30, mwaka huu na majaji hao watatu waliotoa hukumu ya rufaa.
Babu Seya na mwanaye Papii Kocha, Mbangu na Francis walihukumiwa kifungo cha maisha mwaka 2004 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Katika hukumu hiyo ya Juni 25, 2004, Hakimu Mkazi Addy Lyamuya aliwatia hatiani Babu Seya na wanawe watatu kwa makosa 23 ya ubakaji na ulawiti na kuwapa adhabu ya kifungo cha maisha jela.
Baada ya kupewa adhabu hiyo, Babu Seya na wanaye walikata rufani Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, ambapo Jaji Thomas Mihayo (mstaafu kwa sasa), aliwatia hatiani na kuunga mkono hukumu ya Mahakama ya Kisutu, iliyotolewa na Hakimu Lyamuya.
Kutokana na hukumu ya Mahakama Kuu, Babu Seya na wanaye waliamua kwenda Mahakama ya Rufani, ambako Babu Seya na mwanaye Papii Kocha walitiwa hatiani wakati Mbangu na Francis waliachiwa huru.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo , Mahakama iliridhika na ushahidi ulioko kwenye kumbukumbu za mwenendo wa kesi hiyo kwa kila kosa na kwamba mrufani wa kwanza (Babu Seya) na wa pili (Papii Kocha), walihusika katika kutenda makosa. Ilisema utetezi wao kuwa hawakuwepo katika eneo la tukio ulikataliwa.
Katika hukumu hiyo, Babu Seya alitiwa hatiani kwa makosa matano ya kubaka na Papii Kocha alitiwa hatiani kwa makosa mawili.
Chanzo: Habari Leo
No comments:
Post a Comment