Wednesday 4 December 2013

AZAM TV KUANZA DEC 6

KAMPUNI ya Azam Media imezindua rasmi kituo cha televisheni ya Azam TV
‘Burudani kwa Wote’ ambacho kitaanza kuwa hewani kuanzia Desemba 6, mwaka
huu.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam
Media, Rhys Torrington, alisema matangazo hayo yatakuwa yakipatikana

Tanzania nzima na nchi nyingine za Afrika Mashariki kwa kutoa burudani na
vipindi mbalimbali.
Alisema kituo hicho kitakuwa na huduma kutoka chaneli 50 zikiwemo za
kimataifa, za ndani ya Tanzania na tatu kutoka Azam zitakazorusha matangazo
ya Kiswahili, kimataifa na filamu za Kitanzania.

“Kwa kutazama michezo, sinema na matangazo mbalimbali ya miundo ya maisha
mteja wetu atakuwa akilipia sh 12,500 kwa mwezi ili kupata matangazo yetu

kwa ubora na muonekano mzuri,” alisema Torrington.
Torrington alisema kituo hicho kitakuwa kikirusha moja kwa moja Ligi Kuu ya
Bara kupitia chaneli maalumu na kuandaa vipindi mbalimbali kupitia
watayarishaji wake.

Aliongeza kuwa Azam Media iko mbioni kuanzisha kituo cha radio cha Azam FM.

Naye mgeni rasmi katika uzinduzi wa kituo hicho, Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, mbali ya kuipongeza
familia ya Bakhressa kuwekeza katika teknolojia ya utangazaji, alisema
hatua hiyo inadhihirisha Tanzania kuwa mstari wa mbele Afrika katika
mabadiliko ya urushaji wa matangazo ya televisheni kutoka analojia kwenda
dijitali kwa haraka.

Makamba alisema serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Azam Media na
kuzidi kubuni sera nzuri zitakazoongeza uwekezaji katika sekta ya
utangazaji.

Aidha, alitoa changamoto kwa vijana wa Kitanzania wenye vipaji, kuitumia
fursa ya Azam TV kuandaa programu zao na kujiongezea kipato badala ya kukaa
kulaumu na kutuhumu.

No comments:

Post a Comment