Wednesday 18 December 2013

Yanga yaivizia Al Ahly Afrika

KOCHA Mkuu wa Yanga, Ernest Brandts, ametamka kuwa hana wasiwasi na Ligi ya Mabingwa Afrika na kwamba atawachapa Wacomoro kwenye mechi ya kwanza huku akiipigia hesabu kali Al Ahly ya Misri.
Yanga itacheza michuano hiyo mikubwa ya klabu barani Afrika na imepangwa kuanza na Komorozine ya Comoro katika raundi ya kwanza. Mechi zitaanza Februari mwakani. Kama itavuka raundi hiyo, itakutana na Al Ahly katika raundi ya pili, wapinzani hao ndio mabingwa watetezi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Brandts alisema: “Hatuna wasiwasi na ratiba, tutacheza na Wacomoro na baadaye Al Ahly. Siwafahamu hao Wacomoro lakini tumejiandaa kupambana nao, bila shaka itakuwa si timu ya kutisha sana na tunachokifanya sasa ni kuhakikisha tunapata taarifa zao.
“Ninahitaji kuwafahamu kwa kupata mikanda yao ya video, niwaone namna gani wanavyocheza na ni wachezaji gani ni tegemeo lao, kuhusu Al Ahly naifahamu ni timu kubwa, lakini Yanga nao ni kubwa kama unavyojua, siku zote timu nzuri inapangwa na wazuri wenzao kwa maana hiyo hakuna shida, tunajiandaa.
“Lakini kwa sasa Al Ahly nimeiweka pembeni kwanza, ninachoangalia ni huu mchezo wa kwanza na Komorozine, kuona ni namna gani tutapambana nao na kufuzu hatua ya pili na ndipo Al Ahly watafuata.
“Timu ipo vizuri, najivunia hilo kwani hakuna kocha yeyote duniani asiyependa kuwa na timu nzuri. Watu wengi wanajaribu kukiangalia kikosi chetu kwa ajili ya Ligi Kuu pekee, lakini mimi naangalia mbele zaidi hasa mashindano ya kimataifa, lazima tuanze kuweka mikakati sasa.
“Tuna timu nzuri hivyo viongozi wanapaswa kuanza maandalizi kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa ambayo tutashiriki mapema Februari kuhakikisha tunafanya vizuri pia.
“Ubora wa kikosi chetu unatakiwa tuuonyeshe hata kimataifa ili tujitofautishe na wengine kwenye ligi ya ndani, kama tulishindwa huko nyuma kuvuka hatua nyingine tujitahidi sasa kwenda mbele zaidi, naamimi hilo linawezekana kama tutapata maandalizi mazuri.”

No comments:

Post a Comment