Wednesday 18 December 2013

Fufa yaomba msaada Fifa suala la Okwi

SHIRIKISHO la Soka la Uganda (Fufa) limetamka kwamba halina pingamizi dhidi ya Emmanuel Okwi kutua Yanga, lakini katika hali ya kushangaza limeandika barua kwenda Fifa likitaka ufafanuzi kuhusu uhamisho wa mchezaji huyo.
Okwi amesajiliwa Yanga akitokea SC Villa ya Uganda ambayo awali ilimchukua mchezaji huyo kwa mkopo wa miezi sita kutoka Etoile du Sahel ya Tunisia.
Mchezaji huyo aliidhinishwa Villa na Fifa-Shirikisho la Kimataifa la Soka- baada ya kugoma kurudi Etoile ambayo ilikuwa haijamlipa fedha zake za mshahara na marupurupu mengine.
“Tumewaandikia Fifa kwa sababu tunataka watuambie kama uhamisho wake ni sahihi,” alisema Edgar Watson ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Fufa.
Lakini Mwanasheria wa Okwi, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Villa, Edgar Agaba, amesisitiza kwamba kila kitu kiko sawa na Okwi ni mali ya Yanga.
Septemba 28 mwaka huu, Fifa iliiruhusu Fufa kumuidhinisha Okwi kuichezea SC Villa kwa muda wa miezi sita ruhusa ambayo ilitokana na maombi ya Fufa ya Septemba 4 iliyoomba hati ya uhamisho wa kimataifa (ITC) kutoka Shirikisho la Soka la Tunisia ambako Okwi alikuwa akichezea Etoile.
Kwa mujibu wa taarifa ya Fufa iliyosainiwa na Ofisa Habari wake, Rogers Mulindwa, hatua ya Fufa kuomba ITC ya Okwi ilitokana na mchezaji huyo kuilalamikia Etoile baada ya kushindwa kumlipa haki zake ikiwamo mshahara hivyo akaomba kuachana nao ili ajiunge na Villa.
Sakata hilo liliamuliwa na Fifa kupitia Kamati ya Hadhi za Wachezaji chini ya Jaji Geoff Thompson raia wa Uingereza kwa kutoa ruhusa ya mchezaji huyo kupata leseni ya kuichezea Villa kwa muda wa miezi sita.
Hata hivyo, Ofisa Habari wa Fufa, Rogers Mulindwa alisema kwamba Okwi ana uhuru wa kujiunga na timu yoyote kwa kuwa suala lake lilimalizwa na Sahel waliomtoa kwa mkopo Villa ili kulinda kipaji chake.
“Unajua alikuwa na matatizo Sahel na Fifa wakamuidhinisha achezee Villa, sasa baada ya hapo ana haki kucheza Yanga au Simba, mambo mengine yanayoendelea najua ni ushabiki wa ndani kati ya klabu za Tanzania,’’ alisema Mulindwa.

No comments:

Post a Comment