Tuesday 17 December 2013

Okwi awashangaza wachezaji wa Yanga


SAA 24 baada ya Yanga kumsajili mshambuliaji wa zamani wa Simba, Emmanuel Okwi kutoka SC Villa ya Uganda, wachezaji wa timu hiyo wameupa dole gumba uongozi wakisema: “Asanteni kwa kutuletea fundi.”
Wakizungumza na Mwanaspoti mara baada ya mazoezi ya Yanga jana Jumatatu asubuhi kwenye Uwanja wa Bora, Kijitonyama jijini Dar es Salaam, wachezaji hao waliupongeza uongozi kwa kusema Okwi ni mchezaji hodari atakayeongeza ufanisi kikosini mwao.
Mchezaji wa kwanza kuzungumza na Mwanaspoti alikuwa Haruna Niyonzima ambaye alisema amefurahi kuona Okwi amejiunga na Yanga kwani ilikuwa ni ndoto yake ya siku nyingi kucheza na mchezaji huyo.
“Ujue najiona kama naota, kweli Okwi amejiunga na Yanga? Hebu niambie ukweli. Okwi ni mchezaji niliyekuwa nikitamani kucheza naye siku moja, sasa kama kweli amesajiliwa itakuwa poa sana,” alisema Niyonzima.
Straika Jerry Tegete alisema: “Ni mchezaji mzuri anayeweza kuiletea mafanikio Yanga ndani ya muda mfupi, namkaribisha katika timu na nitashirikiana naye kuiletea timu mafanikio.”
Kwa upande wao, beki Juma Abdul na kiungo Frank Domayo, wamesisitiza kwamba kamati ya usajili imefanya uamuzi sahihi na wakasema timu hiyo itatisha kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kipa Juma Kaseja aliyewahi kucheza na Okwi katika kikosi cha Simba kilichoifunga Yanga mabao 5-0 mwaka jana, alisema: “Okwi namjua vizuri, nilicheza naye Simba, Yanga itakuwa vizuri sasa katika safu ya ushambuliaji kwani jamaa (Okwi) ana vitu vingi ambavyo washambuliaji wengine hawana.”
Okwi anatarajiwa kutua nchini wiki hii kujiunga na wenzake wanaojiandaa na mechi ya Nani Mtani Jembe dhidi ya Simba itakayochezwa Jumamosi Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment