Tuesday 17 December 2013

Ningeuza kontena mbili za jezi ya Okwi

YANGA wamepagawa na tukio la saa 24 zilizopita, Emmanuel Okwi ni mchezaji wao. Usishangae Ndio kawaida ya timu zetu. Haijalishi kama kocha anataka au hataki, kitu muhimu ni kumkomoa mtani.
Kuna neno jipya siku hizi linaitwa fursa. Watanzania mmoja mmoja wanalitumia kwa umakini kuliko klabu zetu zinavyoweza kulitumia. Fursa ni kujipatia chochote kwa haraka haraka katika kile ambacho wengine hawajaona.
Kwa mfano, wakati huu huu ambao mashabiki wa Yanga wamepagawa, walipaswa kukimbilia katika maduka ya klabu yao kununua jezi ya Okwi 25. Jezi maridadi kabisa ambayo ingeuzwa kuanzia Sh15,000 kwenda juu.
Lakini iko wapi jezi hii? Duka liko wapi? Hakuna shabiki anayejua. Kinachotokea ni kwamba baada ya muda mfupi wajanja wataingia katika viwanda vya kijanjajanja Kariakoo na kutoa jezi zao feki ambazo hazina uhusiano na klabu.
Nasikia mchezaji mwenyewe amechota dola 60,000. Klabu yake SC Villa imechota dola 20,000. Kwa nini mchezaji asirudishe kiasi walau nusu ya kiasi kilichotumika kwa mauzo ya jezi na vifaa vinavyoambatana na jina lake wakati huu mashabiki wakiwa wameingia wazimu kwa ujio wake?
Hapa ndipo soka la Tanzania lilipopotea tangu miaka mingi iliyopita. Kila kitu kinaendelea kufanywa kama burudani tu. Kinafurahisha nafsi za mashabiki kwa macho tu, lakini klabu maarufu zenye mashabiki zaidi ya milioni tano nchi nzima zinaendelea kuishi kwa hisani ya watu wachache.
Wakati Arsenal wakimpima afya Mesut Ozil kabla hajamalizia kusaini mkataba wa timu yao, tayari klabu ilikuwa inaanza kuchapisha jezi yake namba 11 kwa ajili ya kuanza kupunguza maumivu ya kumnunua mchezaji huyo kwa bei mbaya.
Nisingeshauri hili kama ningekuwa raia wa Kenya ambako siasa inapendwa zaidi kuliko soka. Lakini katika nchi yenye wazimu kama hii, mchezaji kama Okwi anaweza kutumika katika kutengeneza noti nyingi klabuni.
Hapa naizungumzia nchi maskini yenye wazimu wa soka inayopatikana katika dunia ya tatu. Hata hivyo bado tunatupa pesa jalalani na kulalamika kwamba maisha yamekuwa magumu.
Matokeo yake, mpaka leo, mchezaji anasajiliwa kwa gharama ya dola 80,000 kwa jumla lakini ataenda kufanya mazoezi katika uwanja mbovu wa Loyola. Klabu haiwezi kujitegemea kwa kutengeneza uwanja wa kisasa wa mazoezi.
Na kama uwanja ule ule wa Kaunda ungekuwa umetengamaa, wiki ya kwanza ya mazoezi ya Okwi na Yanga ingeingiza kiasi cha Sh 10 Milioni. Hizi ni hesabu za wenzetu wenye akili ya kibiashara zaidi kuliko ya kutegemea mifuko ya watu.
Lakini kwa sasa watu wanaopiga pesa nyingi zaidi kwa ujio wa Okwi Yanga ni kampuni za magazeti kuliko timu yenyewe. Jina lake litatumika kutengeneza pesa nzuri kwa siku nyingi zijazo hasa ukizingatia kuwa hata klabu zenyewe hazina magazeti yaliyotengamaa kuitengeneza habari na kuiuza.
Natabiri kuwa tutaendelea kutegemea wahisani kwa miaka mingi ijayo kama hatuwezi kuwa na akili ya haraka ya kutumia rasilimali watu. Kila siku mchezo wa soka utakuwa unaburudisha mioyo yetu tu, lakini hatutaweza kuutumia katika kutengeneza pesa.
Kwa wenzetu usajili kama huu ungeinufaisha klabu, Mmachinga, shabiki wa kawaida na kila mtu. Sisi unamnufaisha mchezaji peke yake.

Mwanaspoti

No comments:

Post a Comment