Saturday 14 December 2013

Hali tete baraza la mawaziri

Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete, imeanza kuwahoji mawaziri waliotajwa ni ‘mzigo’ kwa Serikali.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, jana alilithibitishia gazeti dada la Mwananchi, The Citizen juu ya kuanza kwa kikao cha Kamati Kuu (CC), lakini hakuwa tayari kuingia kwa undani kuhusu ajenda.
Hata hivyo, habari za ndani zilieleza kwamba miongoni mwa ajenda kuu za CC ni kuwahoji mawaziri wanaolalamikiwa na wananchi, kwamba wameshindwa kutekeleza majukumu yao.
Wakiwa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Nape aliwatupia lawama mawaziri wakati akielezea changamoto zinazowakabili wakulima ambao ni asilimia 80 ya Watanzania, huku mawaziri husika wakikaa kimya.
Mawaziri waliotajwa mzigo ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza na Naibu wake, Adam Malima, kwamba wameshindwa kazi na alipendekeza wang’olewe.
Hata hivyo, gazeti hili jana lilishuhudia mawaziri kadhaa wakifika na kuingia kwenye mkutano wa CC, taarifa zingine zilisema mawaziri waliofika kwenye kikao hicho walihojiwa na wajumbe wa CC.
Kuhojiwa na CC
Mawaziri waliohojiwa na CC hadi kufikia saa 8:00 mchana jana walitajwa kuwa ni Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza. Mkuya ndiye ambaye kwa sasa anaisimamia Wizara Fedha kutokana na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa kulazwa nchini Afrika Kusini akisumbuliwa na maradhi ambayo hayajatajwa.
Waandishi wa gazeti hili jana waliwashuhudia takriban mawaziri 10 wakiingia katika ofisi za makao makuu ya CCM, Dodoma, maarufu White House, huku baadhi wakiwa si wajumbe wa CC.
Habari zilizotufikia jioni ziliwataja wengine kuwa ni Dk David Mathayo David (Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi), Hawa Ghasia (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-Tamisemi), Dk Kawambwa, Celina Kombani (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma).
Dk Kawambwa wakati akitoka kwenye kikao cha CC aliulizwa na waandishi wa habari kilichotokea na yeye alijibu kwa kifupi; “Mawaziri mizigo ndiyo tunatoka.”
Mawaziri ambao si wajumbe wa CC ni Mkuya, Chiza, Dk Kawambwa, Hawa Ghasia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Utawala Bora, George Mkuchika ambaye naye taarifa zilidai alihojiwa.
Azimio la Bunge
Tayari Bunge limepitisha azimio la kumtaka Ghasia pamoja na naibu mawaziri wake wawili, Aggrey Mwanry na Majaliwa Kassim Majaliwa, kupima na kutafakari kama bado wanatosha kusimamia wizara hiyo.
Kiini cha Bunge kupitisha azimio hilo ni taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kubainisha kuwapo wizi, ubadhirifu na mtandao wa ufisadi ndani ya Tamisemi, Halmashauri na Hazina.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye baadhi ya wabunge wamemtaja kama waziri mzigo namba moja, amesema yuko tayari kuachia ngazi kama Rais ataamua kumwondoa katika wadhifa huo.
Pinda alitoa kauli hiyo juzi bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la papo kwa hapo kutoka kwa Mbunge wa Viti Maalumu, Rukia Ahmed (Cuf) aliyetaka aeleze anajisikiaje kuitwa mzigo namba moja.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema yeye anasimamia wizara 20, hivyo kama wapo watakaomhukumu kwa sababu ya wizara moja ama mbili kutofanya vizuri basi watu hao watakuwa hawamtendei haki.
Alisema kama Rais atamwona ameshindwa kuwajibika yuko tayari kuachia ngazi na endapo Rais hatafanya hivyo na wabunge bado wakaona ipo haja hiyo, wampigie kura ya kutokuwa na imani naye.
Kauli ya CCM
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, mbele ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, alisema kuwa mawaziri hao wameshindwa kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia Watanzania.
Alisema kuwa Waziri Chiza na Malima wamebaki wakifunga tai na kuvaa suti mjini wakati wakulima wa Ruvuma na mikoa mingine ya Tanzania wakiteseka.
Nape alisema Waziri Kawambwa naye anatakiwa kuchukuliwa hatua kwa kuingia mkataba na kampuni ya ujenzi ya Progressive iliyopewa zabuni ya kutengeneza barabara ya Namtumbo hadi Tunduru wakati mkandarasi huyo hana uwezo wa kuijenga na matokeo yake amefukuzwa kazi.
Dk Kawambwa ametupiwa lawama hizo kutokana na kuipa kazi kampuni hiyo wakati akiwa Waziri wa Miundombinu pamoja na kushindwa kusimamia elimu.

Mwananchi

No comments:

Post a Comment