Saturday 14 December 2013

MPASUKO FAMILIA YA MANDELA

HOFU kuu iliyopo sasa nchini Afrika Kusini kufuatia kifo cha aliyekuwa rais wa kwanza mweusi, Nelson Mandela ‘Mzee Madiba’ ni kupasuka kwa familia yake baada ya mazishi yatakayofanyika kesho kijijini Qunu, Eastern Cape Mkoa wa Mthatha.
Baadhi ya wananchi nchini humo wameonesha wasiwasi wao kuhusu hatima ya mjane wa marehemu Mandela, Graca Machel kwamba, huenda akatengwa kutokana na umbali wa ujamii.
Graca ni mzaliwa wa Msumbiji. Aliwahi kuwa mke wa Rais wa Kwanza wa Msumbiji, hayati Samora Moses Machel. Pia amewahi kuwa Waziri wa Elimu wa Msumbiji.
Mandela akiwa na Graca.
 HAKI YA KUMILIKI MALI
Mtandao mmoja nchini humo ulidai kwamba, haki ya kumiliki mali za marehemu ipo kwa msemaji mkubwa wa familia ya Mandela, Mandla Makgatho Mandela (39) ambaye ni mjukuu wa kwanza wa marehemu.
Mandla ndiye aliyekabidhiwa mwili wa marehemu na wanajeshi waliobeba jeneza siku ulipopelekwa kwenye Jengo la Muungano, Pretoria nchini humo.
Mbali na dereva, mtu mwingine aliyekuwa ndani ya gari lililobeba jeneza ni Mandla.
Mandela akiwa na Winne.
SIFA YA MANDLA
Mandla anatajwa kuwa msemaji mwenye mamlaka ya kufanya lolote kutokana na wadhifa wake huo ambao hautenguliki kimila. Hata marehemu alilijua hilo.
MASWALI YA WATU
Maswali mengi ya wakazi wa nchi hiyo ni kama Mandla ataweza kumchukulia Graca kuwa ni mjane sahihi anayestahili kupata haki sawa.
Mandla (katikati) akiwa na familia.
KUMBUKUMBU
Kabla ya kifo cha Mandela, Mandla aliwahi kuingia matatani na baadhi ya watoto wa marehemu kufuatia kitendo chake cha kuhamisha miili ya marehemu wa ukoo huo kutoka Qunu kwenda kuizika upya anakoishi hali iliyotafsiriwa kuwa, alitaka Mandela akifa akazikwe huko Nvezo.
Ndugu mbalimbali walikuja juu na kumtaka arudishe miili hiyo Qunu la sivyo sheria ingetumika.
“Hatudhani kama Mandla ataweza kumbeba Graca kama mjane sahihi wa Mandela, wala hatudhani kama familia hiyo itasimama kwa amani baada ya kifo cha Madiba,” ilisema sehemu ya mtandao huo ikimkariri mmoja wa raia wa nchi hiyo.
UWEPO WA WINNIE WATIA SHAKA
Habari zaidi zilidai kuwa, uwepo wa Winnie Mandela ambaye aliwahi kuwa mke wa marehemu kabla ya kutengana baada ya kutoka jela mwaka 1990, ni chachu ya kuweza kuwepo kwa mpasuko huo kwa sababu ana watoto ambao hawaungi kizazi cha Mandla.
Mandla alizaliwa kwa mke wa kwanza wa Mandela, Evelyn Mase Mandela hivyo ni rahisi uzao wa Winnie kuwa na msimamo tofauti na msemaji huyo.
NGUVU YA WINNIE NA GRACA
Nchini Afrika Kusini, Graca ametokea kuwa na nguvu zaidi ya Winnie akichukuliwa kuwa ndiye aliyemtunza mzee Madiba katika kipidni chake cha uzee, kutoka gerezani hadi kifo.
Winnie, yeye zaidi ya kuwa katika harakati za kupigania uhuru wakati Mandela akiwa gerezani, alichafuka na skendo yake ya usaliti hivyo kukosa mvuto kwa jamii ya nchi hiyo.
MANDELA ANAZIKWA KESHO
Merehemu Mandela atazikwa kesho kijijini kwake, Qunu ambako maelfu ya watu wanatarajiwa kuhudhuria.

GPL

No comments:

Post a Comment