Monday 2 December 2013

Bunge lamwondoa Waziri Mkuu Somalia


Waziri Mkuu wa Somalia Abdi Farah Shirdon amepigiwa kura ya kutokuwa na imani naye na Bunge la nchi hiyo kwa wingi wa kura.
Hii ina maana Waziri Mkuu huyo atakuwa amekaa kwenye nafasi hiyo kwa miezi 15 tu tangu ateuliwe kushika wadhifa.Bwana Shirdon aliingia katika mgogoro na rais wa nchi hiyo Hassan Sheikh Mohamud mwezi uliopita baada ya Waziri Mkuu huyo kujaribu kuwafuta kazi mawaziri wanaoungwa mkono na Rais Mohamud.
Rais Mohamud aliingia madarakani mwaka 2012 ikiwa ni jitihada za Umoja wa Mataifa kumaliza mgogoro nchini humo.
Wabunge waliopiga kura ya kutokuwa na imani naye ni wabuge 184 dhidi ya 65.
Somalia imekuwa katika mgogoro na vita vya muda mrefu dhidi ya wapiganaji wa kiislam wa Al shabaab. Hata hivyo bado kundi la Al Shabaab linaendelea kushikilia maeneo mengi nchini Somalia.
Majeshi ya serikali yakishirikiana na Umoja wa Mataifa AMISOM yamekuwa yakiwaondoa wapiganaji hao wa Al Shabaab katika baadhi ya miji mikubwa kwa miezi 18 sasa. Japo kundi hilo limekuwa likiendelea kundesha mashambulizi ya mara kwa mara.
Mchambuzi wa BBC wa masuala ya Somalia Abdullahi Abdi Sheik amesema hatua ya waziri mkuu huyo kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye huenda ikamaliza mvutano wa kiungozi kati yake na Rais wa nchi hiyo jambo lililosababisha baadhi ya shughuli za serikali kukwama.
Baada ya kura hiyo ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, sasa rais wa nchi hiyo atakuwa na siku 30 kumteua Waziri Mkuu mpya.

No comments:

Post a Comment