Sunday 15 December 2013

Okwi asaini Yanga miaka miwili


YANGA imefanya umafia, imemsajili mshambuliaji wa zamani wa Simba, Emmanuel Okwi kwa mkataba wa miaka miwili na nusu na huenda akaichezea timu hiyo Jumamosi ijayo katika mechi ya Mtani Jembe dhidi ya Simba, Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Abdallah Bin Kleb aliliambia Mwanaspoti jana Jumapili jioni kuwa mshambuliaji huyo amesaini mkataba wa miaka miwili na nusu.
“Kaka ni kweli tumemsajili Okwi, tumepata mpaka ITC yake. Sisi tumemsajili kutoka SC Villa ya Uganda,” alisema Bin Kleb.
Bin Kleb alifafanua kuwa katika suala hilo wamemshirikisha meneja wa Okwi, wakala wake na mwanasheria na kwamba mikataba yote imesainiwa.
Usajili huo ni wazi kwamba utawashangaza mahasimu wao, Simba ambao walikuwa na mgogoro na mchezaji huyo na klabu waliyomuuza ya Etoile du Sahel ya Tunisia kwa ada ya Dola 300,000 (Sh 480 milioni) fedha ambazo bado hawajalipwa mpaka sasa.
Hata hivyo wakati Simba wakiwa katika mgogoro huo, Yanga wameibuka na kumsajili mchezaji huyo jana Jumapili saa chache kabla ya muda uliowekwa na TFF kwa klabu kukamilisha usajili wa wachezaji wa Ligi Kuu Bara. Klabu zote za Ligi Kuu zilitakiwa kufanya kusajili wa wachezaji wapya kuanzia Novemba 15 hadi Desemba 15 saa sita usiku (jana Jumapili).
Okwi kwa mara ya kwanza alisajiliwa na Simba mwaka 2010 akitokea Sports Club Villa ya Uganda kabla ya kumuuza Sahel Januari mwaka huu lakini tangu Simba wamuuze suala la malipo limekuwa gumu huku Okwi mwenyewe akilalamika kuidai klabu hiyo mishahara na marupurupu.
Kutokana na hali hiyo alikubali kusaini SC Villa mkataba wa miezi sita baada ya klabu hiyo kuomba kibali maalumu Fifa ili kumtumia kwa lengo kuokoa kipaji chake jambo ambalo viongozi wa Simba walilipinga na kuahidi kulikatia rufaa Fifa.
Kwa kipindi kirefu Kocha wa Yanga, Ernest Brandts amekuwa akilalamika kutoridhishwa na safu yake ya ushambuliaji na ni wazi kwamba usajili wa mshambuliaji huyo utakuwa umemfariji Brandts na atamtumia vyema kwenye Ligi Kuu Bara mzunguko wa pili na mashindano ya kimataifa.

Mwanaspoti

No comments:

Post a Comment