GHANA imepiga hatua kubwa kuelekea fainali za Kombe la Dunia
zitakazofanyika Brazil mwakani baada ya kuikandamiza Misri mabao 6-1
katika mechi ya kwanza ya mchujo ya kuwania kushiriki fainali hizo
uliochezwa juzi Jumanne mjini Kumasi, Ghana.
Asamoah Gyan alifunga bao la kwanza kabla ya Ghana
kuongoza 2-0 baada ya kiungo Michael Essien kumsababishia beki Wael
Gomaa ajifunge mwenyewe.
Misri ilipunguza moja kwa mkwaju wa penalti ya
Mohamed Aboutrika, lakini Black Stars ilikuwa na siku njema baada ya
Majeed Waris kufunga kwa kichwa kufanya ubao wa matokeo usomeke 3-1 na
Gyan akaongeza bao lake la pili likiwa la nne kwa wenyeji.
Kiungo anayecheza soka AC Milan kwenye Serie A,
Sulley Muntari, aliifungia Ghana kwa mkwaju wa penalti kabla ya
Christian Atsu kukamilisha hesabu na kuifanya timu hiyo kwenda kwenye
mechi ya marudiano itakayofanyika Cairo, Misri iliwa na faida kubwa ya
mabao.
Kwa matokeo hayo, Ghana imekuwa na uhakika mkubwa
kwamba itapanda ndege kwenda Amerika Kusini mwakani kwenye fainali hizo
za Brazil.
No comments:
Post a Comment