Thursday, 17 October 2013

‘Nitazaa watoto wawili, baba yao siri yangu’


MIAKA tisa imepita tangu kipaji cha uimbaji cha mwanamuziki Sarah Kaisi ‘Shaa’ kilipoibuliwa katika mashindano ya Coca Cola Pop Star akiwa na Witness Mwaijaga na Langa Kileo (marehemu). Mwanamuziki huyo anasema alipoanza kuwika katika muziki,  alijiwekea malengo, moja kati ya hayo ilikuwa ni kuanzisha familia. Yatuatayo ni mahojiano baina yake na Mwanaspoti yaliyofanyika hivi karibuni.
Mwanaspoti: ‘Ni mipango gani ulijiwekea mara baada ya jina lako kuanza kuwika katika Bongo flava?
Shaa: Mikakati yangu ilikuwa ni kufanya muziki kwa kipindi cha miaka saba ndipo nianzishe familia ambayo itakuwa na watoto wawili. Lakini sasa imefika miaka tisa ndoto haijatimia. Kuna sababu mbalimbali ambazo bado nazifanyia kazi.
Nilipanga nikishazaa niwaangalie kwa karibu watoto kwa malezi huku nikiendelea na kazi yangu ya muziki. Sikuhitaji kupata watoto mapema, mimi kama Shaa naamini kuwa mtoto anakuja kwa kupanga, siwezi kuzaa watoto mapema kisha nikawalaza njaa.
Mwanaspoti: Ni kitu gani kinakukwamisha katika kuanzisha familia, hujampata mtarajiwa?
Shaa: Kiukweli mtarajiwa wangu siwezi kumwanika kwani kwa sasa jina lake bado ni siri yangu, mtamjua tu mambo mazuri hayataki haraka.
Mwanaspoti lilitaka kujua mengi kutoka kwa mwanamuziki huyu anayetamba na wimbo wa ‘Lavalava’  hasa baada ya kuwapo tetesi kwamba amejiunga na sehemu ya Kundi la Wanaume Family yaani kituo cha Mkubwa na Wanawe kilicho chini ya Said Fella.
Mwanaspoti: Shaa, kuna tetesi kwamba sasa umejiunga katika moja ya matawi ya Wanaume Family, kuna ukweli wowote katika hili?
Shaa: Mimi ni msanii katika lebo ya MJ Records kwa kipindi cha miaka minne sasa. Lakini hivi karibuni nimekuwa nikisimamiwa na mameneja mbalimbali wakiwamo AY na baadaye nilianza kusimamiwa na Babu Tale.
Nimekuwa kwa Tale kwa kipindi kirefu sasa lakini yeye akaona si mbaya kama akimwingiza Fella naye ili kuukuza zaidi muziki wangu.
Mwanaspoti: Katika Kundi la TMK umesaini mkataba wa aina gani?
Shaa: Mkataba wangu ni wa miezi sita tu. Nikiwa TMK nitakuwa nikiwafundisha muziki vijana wa kituo cha Mkubwa na Wanawe na nitafanya nao kazi angalau mbili za muziki. Mfano sasa nimesharekodi kazi inayoitwa ‘Sugua Gaga’, kazi hii nimefanya na watoto wa kituo cha Mkubwa na Wanawe na inatarajiwa kuachiwa katika vituo mbalimbali vya redio wiki ijayo, huku video ya wimbo huo ikiwa inapikwa jikoni.

Mwanaspoti: Wimbo huo unazungumzia nini hasa?
Shaa: Sugua Gaga imeimbwa kama sehemu ya kuwapa motisha watu kutokata tamaa ya maisha. Unajua shida zipo duniani hivyo mtu unapokutana na vikwazo haimaanishi uache kazi unayoifanya au ugeukie pembeni na kuacha ulilokuwa unafanya.
Ukikutana na hali hiyo unachotakiwa kufanya ni kufuta vumbi na kusonga mbele. Lakini si huo tu kuna kazi nyingi zinakuja nilizofanya nikiwa na AT, Shetta na wengineo.
Mwanaspoti: Nini kilichosababisha ushindwe kutokea katika shoo kwa siku za hivi karibuni.
Shaa: Sikuweza kufika kwenye shoo kutokana na machungu niliyokuwa nayo kutokana na kuuguza na baadaye msiba wa mama yangu.
Mwanaspoti: Unakumbuka nini kutoka kwa mama yako na ni kauli gani alikusisitizia kabla hajapatwa na umauti.
Shaa: Mama alinisisitiza sana kuwa na watoto. Hilo ndilo tamko lake alilolitoa mara kwa mara hasa kipindi cha miezi mitatu ya mwisho tulipokuwa tukimuuguza. Alipenda sana kusema kwamba anapata watu wa kumuuguza kwa kuwa alizaa hilo ndilo nitakalolikumbuka daima.
Mwanaspoti: Ili kuchukua muda gani kuendelea na shughuli zako za muziki baada ya kifo cha mama yako?
Shaa: Mimi ni binadamu, nilikuwa na uchungu usio kawaida, ilinichukua kama miezi miwili hivi kukaa sawa. Ndio kwanza ninaanza kurudi katika hali yangu ya awali.
Mwanaspoti: Nini ambacho hutakisahau kutoka kwake?
Shaa: Upendo na ukarimu. Inajulikana kila mama lazima anampenda mwanaye, lakini mama yangu alikuwa na utofauti sana katika hili, siku zake za mwisho kama watoto wake tulipata nafasi ya kukaa naye alituusia mengi na alituacha vizuri.
Sina sababu ya kufafanua katika hili ila alituacha vizuri, baada ya kifo chake tulikuwa na uchungu uliochanganyika na faraja.

No comments:

Post a Comment