SERIKALI ya Zambia imetoa hati ya kukamatwa kwa wanasoka watatu
wa nchi hiyo ambao walikosa mechi ya kirafiki wakati Chipolopolo
iliponyukwa mabao 2-0 na Brazil juzi Jumanne.
Wanasoka hao ni wale wanaochezea klabu ya TP
Mazembe ya DR Congo ambao ni Rainford Kalaba, Stoppila Sunzu pamoja na
Nathan Sinkala.
Wote hawakucheza mechi hiyo kwa madai kuwa ni
majeruhi, madai ambayo yalilikera Shirikisho la Soka la Zambia na hivyo
serikali ya nchi hiyo kuamua kuingilia.
Baada ya wachezaji hao kusafirishwa kwa ndege ya
kukodi kutoka DR Congo hadi Lusaka Zambia ili kufanyiwa vipimo kama
kweli ni wagonjwa, shirikisho hilo la Zambia lilisema bado walipaswa
kwenda kwenye kambi ya timu iliyokuwa Beijing, China walikomenyana na
Brazil, lakini Mazembe iliwataka warudi DR Congo na wakafanya hivyo.
Jambo hilo liliichukiza Serikali ya Zambia na
kuwanyang’anya pasi za kusafiria ili tu wasiweza kurudi Lubumbashi
kuungana na klabu yao.
Lakini wachezaji waliweza kupenya kwenye mpaka wa nchi hizo mbili na inaaminika kwa sasa wapo DR Congo.
Shirikisho la Soka la Zambia limeiandikia barua
Fifa likiilalamikia Mazembe kwa kugoma kuwaruhusu wachezaji hao
walipohitajika kwa ajili ya mechi za kimataifa. Kwenye mechi ya kirafiki
iliyopigwa Beijing, kikosi cha Zambia kilifungwa mabao 2-0 yaliyowekwa
kimiani na Oscar na Dede ikiwa ni mechi ya kwanza kwa nchi hiyo
kumenyana na Brazil. Mechi hiyo pia ilikuwa ya kwanza kwa kocha wa muda,
Patrice Beaumelle, 35, aliyechukua mikoba ya Herve Renard aliyetimka
siku 10 zilizopita kufutia Zambia kufeli kuingia katika mchujo wa kusaka
tiketi ya fainali za Kombe la Dunia.
No comments:
Post a Comment