Thursday, 17 October 2013

VIONGOZI WAWE MAKINI KUTOA KAULI,MAAMUZI YAO


  Hivi karibuni viongozi mbalimbali wa Chama na serikali wamekaririwa wakitoa kauli zenye mkanganyiko na maamuzi mbalimbali ambayo yameacha sintofahamu kwa wananchi.Kiongozi mzuri ni yule anayeheshimu utawala wa sheria na hivyo kuzingatia taratibu na sheria zilizowekwa ambazo yeye ana wajibu wa kuzisimamia wakati wa kutoa maamuzi mbalimbali, hususan yanayowagusa wananchi moja kwa moja.

Zipo kauli tata ambazo zimewahi kutolewa na viongozi mbalimbali, ikiwamo ile ya kila mtu atauchukua mzigo wake mwenyewe, wakikaidi amri halali wapigwe tu, ikibidi kula nyasi mtakula lakini ndege ya Rais lazima inunuliwe, hivi ni vijisenti tu, asiyeweza kulipa nauli mpya kigamboni apige mbizi ndiyo nilitumia helikopta ya jeshi kwenda nayo kwetu Urambo Mlitaka nipande punda?
Kauli tata nyingine ni wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam wanafikiria kwa kutumia makalio, foleni Dar es Salaam ni ishara ya maisha bora, mnauliza mvua kwani mimi ni waziri wa mvua, acheni wivu wa kike na wapo walioenda mbali zaidi na kutoa lugha chafu wakati vikao vya bunge vikiendelea huku wakionekana moja kwa moja kwenye runinga.
Kwa siku kadhaa zilizopita mpaka sasa nimekuwa nikafuatilia kwa karibu matukio mbalimbali yanayojiri katika ziara ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bw. Abdallah Bulembo, anayoifanya katika wilaya zote za Mkoa wa Tanga.
Miongoni mwa yaliyojiri katika ziara ya Mwenyekiti huyu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa wa Chama Cha Mapinduzi; ni agizo lake la kuwarudisha nyumbani wanafunzi 21 wakiwemo wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Kideleko, iliyopo wilayani Handeni kwa kushindwa kulipa ada.
Ambapo alikaririwa akisema "huwezi kufuta sifuri kama wanafunzi wanaenda shule na kushindwa kulipa ada, kwani ada hiyo ndiyo inawezesha shule kujiendesha, hivyo wanafunzi wote wanaodaiwa warudi nyumbani hdi watakapopata ada."
Aidha, Bw. Bulembo aliahidi shilingi laki 5 kwa kila mwanafunzi wa shule za Jumuiya ya Wazazi atakayemaliza kidato cha nne na kupata daraja la kwanza; na kuwaagiza wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kwemvumo,iliyopo kata ya Mponde, tarafa ya Soni wilayani Lushoto, waandamane hadi ofisini kwa mkuu wa shule iwapo dakika tano zitapita mwalimu hajaingia darasani.
Na kusisitiza kuwa kuanzia mwakani ada ya shule za Jumuiya ya Wazazi zitapanda kutoka viwango vya sasa shilingi 650,000 hadi shilingi milioni 1.2 (bweni) na shilingi 350,000 hadi shilingi 600,000 (kutwa) na lengo likiwa ni kufuta daraja la sifuri, ambapo yeye anaamini kwa kuongeza ada ufaulu utaongezeka, jambo ambalo huenda likawa na mada pana tukizitazama shule za kata ambazo ada yake ni ya bei nafuu.
Wakati akiendelea na ziara yake, mwanzoni mwa wiki hii Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Wazazi Taifa ya Chama Cha mapinduzi akihutubia mkutano wa hadhara kata ya Duge, wilayani Tanga amekaririwa na vyombo vya habari akimtaka Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, aache kukurupuka na kuingilia uhuru wa wananchi kutoa maoni ya katiba na kusisitiza kuwa msimamo wa Chama Cha Mapinduzi ni serikali mbili.
Hali hiyo ilipelekea Tume ya Mabadiliko ya Katiba kupitia kwa mwenyekiti wake, kujibu shutuma hizo kwa kuwataka wanasiasa kujadili rasimu iliyotolewa badala ya kuhangaika na tume au wajumbe wake.
Aidha, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Nape Nnauye naye alilazimika kutoa ufafanuzi ya kwamba Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa wa Chama Cha Mapinduzi Abdallah Bulembo hakutumwa na CCM kuishambulia na kuishutumu Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Jaji Warioba kwa kuwa si msemaji wa chama hicho na kuitaka jamii na Tume hiyo ielewe kwamba hayo yalikuwa ni mawazo yake binafsi.
Mbali na baadhi ya matukio niliyoyataja hapo awali, nimelazimika kuchukua kalamu na kuandika makala haya baada ya kusoma gazeti la Majira toleo namba 7210 la Jumatano Oktoba 2, 2013 na kuguswa habari iliyobebwa na kichwa cha habari kinachosema "Bulembo afukuza mwalimu."
  Nilivutiwa na habari hii na kutaka kufahamu kwa undani nini hasa kilichojiri na kupelekea mwalimu huyu kufukuzwa kazi.Akiendelea na ziara yake mkoani Tanga, Bw. Bulembo alitoa agizo kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Boza iliyopo wilayani Pangani,mkoani Tanga Bw.Gideon Masue kumfukuza kazi Mwalimu Salmini Mmari kwa kile alichodai mwalimu huyo kukosa busara, ustaarabu na kujaa dharau, baada ya kukataa kutaja kiwango chake cha mshahara mbele ya Bodi ya shule,walimu na baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi mkoa na wilaya waliokuwepo ukumbini.
  Kimsingi hata kama Shule ya Sekondari Boza inamilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi ambayo Bw. Bulembo ndiye Mwenyekiti wake, bado mwalimu Salmin Mmari ilikuwa sahihi kwa kukataa kutaja kiwango cha mshahara wake hadharani na Bw. Bulembo hana mamlaka ya kumlazimisha afanye hivyo.
  Aidha, uongozi wa Jumuiya ya Wazazi Taifa ya Chama Cha Mapinduzi na bodi ya Shule ya Sekondari Boza kwa ujumla wao hawana mamlaka ya kutaja hadharani mshahara wa mwalimu huyo kwa mujibu wa Sheria ya kazi ya mwaka 2004, kifungu cha 70, kifungu kidogo (2)(d) kinachozuia mwajiri kutoa taarifa binafsi za mwajiriwa bila ya ridhaa yake.
  Jumuiya ya Wazazi kama mwajiri inaweza kutangaza viwango vya mishahara vya walimu wanaofundisha katika shule zake kwa ujumla wake, lakini si kwa mwalimu mmoja mmoja mathalan kutaja hadharani kuwa mwalimu Mmari mshahara wake na marupurupu mengine ni kiasi fulani.
  Sheria ya Kazi kifungu cha 27 kifungu kidogo (1)(c) kimeainisha wazi kuwa malipo ya mshahara iwapo yanafanyika kwa fedha taslimu au hundi, yalipwe kwenye bahasha iliyofungwa, na hii inadhihirisha wazi kuwa mshahara wa mtu ni siri kati ya mwajiri na mwajiriwa.
  Mwajiriwa ni tofauti na kibarua, kwa kuwa kwa upande wa vibarua inajulikana wazi kuwa kwa kutwa wanalipwa kiasi fulani, hivyo hata ukiwapanga foleni na kumpa kila mtu hela yake mkononi si tatizo, lakini tunapokuja kwa upande wa mwajiriwa hali ni tofauti na ndio maana Sheria inamtaka mwajiri kutoa malipo kwa staha, ikiwemo fedha taslimu na mchanganuo wake ndani ya bahasha iliyofungwa, hundi na mchanganuo wake, au mchanganuo 'bank slip' uliofungwa kama fedha hizo zimewekwa katika akaunti ya mwajiriwa.
  Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa wa Chama Cha Mapinduzi ameonyesha udhaifu mkubwa katika mambo mawili, mosi kitendo cha kumtaka Mwalimu Mmari ataje mshahara wake hadharani hakikuwa sahihi na naungana na mwalimu huyo kwa ujasiri aliounyesha wa kukataa kufanya hivyo.
  Pili kitendo cha kumfukuza kazi mwalimu 'kiholela' bila ya kufuata utaratibu si cha kiungwana, kwa mujibu wa sheria za kazi; yapo makosa ambayo yanaweza kusababisha mtu afukuzwe kazi lakini si hili la kumtaka mtu bila ya ridhaa yake atoe taarifa zake binafs; na mbaya zaidi Mwalimu Mmari hakupewa muda wa kujitetea.
  Mwalimu Mmari ambaye kwa mujibu wa maelezo yake amefundisha shule hiyo kwa miaka 13 mfululizo hakutendewa haki; na hii inadhihirisha ni jinsi gani mchango wa walimu hauthaminiwi, mtu ambaye amejitolea miaka 13 anafukuzwa kazi kwa kudhalilishwa, cha kushangaza mpaka sasa sijasikia tamko lolote kutoka kwa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) wala kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kuhusiana na uonevu huu.
  Mbali na kusikia mwalimu huyu akikaririwa akisema kuwa anajutia kitendo chake cha kukataa kutaja mshahara wake, kwani hakujua kama anakosea kwa kuwa anaamini mshahara ni siri kati ya mwajiri na mwajiriwa, na kama akipata nafasi ya kujitetea atafanya hivyo.
  Naamini Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kinawajibika moja kwa moja katika kumtetea mwalimu huyu, ambaye pamoja na utumishi wake kwa kipindi cha miaka 13 lakini bado mchango wake haukuthaminiwa na hii itawavunja moyo walimu wengine, ambao wengi wao wanafanya kazi katika mazingira magumu ikiwemo ukosefu wa nyumba za kuishi, uhaba wa vitendeakazi, kipato duni, hali kadhalika kufundisha idadi kubwa ya wanafunzi.
  Viongozi ni kioo cha jamii na hivyo wanapaswa kuchukua tahadhari kabla ya kutoa kauli, maamuzi hadharani, kwa kuwa huenda wananchi wakatafsiri isivyo na hii ikapelekea chuki katika ya wananchi na viongozi, hivyo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi bado ana nafasi ya kutafakari kauli zake na uamuzi wake wa kutoa agizo la kumfukuza kazi mwalimu huyu kabla hajachelewa.
  Aidha, kiongozi anapoamua kutoa maoni yake kuhusiana na jambo lolote kama vile Katiba Mpya, ni muhimu akaweka wazi kuwa anachofanya ni kutoa maoni yake binafsi na si maoni ya jumuiya au chama, kwa kuwa naamini hata wanachama wa Jumuiya au vyama wana haki ya kutoa maoni yao binafsi, kwani hiyo ndio demokrasia ya kweli

No comments:

Post a Comment