Monday 11 November 2013

Al-Ahly baba lao Afrika

MABINGWA watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al-Ahly ya Misri jana Jumapili walifanikiwa kulitetea taji hilo baada ya kuichapa Orlando Pirates ya Afrika Kusini mabao 2-0 mechi iliyopigwa katika Uwanja wa Arab Contractors, Cairo.
Mohammed Aboutrika aliipatia Ahly bao la kwanza dakika ya 54 akiitumia vizuri pasi ya Abdullah Said ambaye mpira alioupiga ulimbabatiza Gcaba kabla ya kumkuta mfungaji. Kuingia kwa bao hilo kuliongeza ushindani kwa timu zote lakini ni juhudi za Ahly zilizozaa bao dakika ya 78 mfungaji akiwa ni Ahmed Abdul Zaher aliyeinasa pasi ya Ahmed Fathy.
Pirates ndio walioanza kwa kasi mechi hiyo, dakika ya tatu tu walifanya shambulizi, Segolela alifumua shuti lakini mpira huo uliokolewa kiulaini na kipa wa Ahly, Ekramy.
Katika mechi ya kwanza ambayo Ahly walikuwa ugenini matokeo yalikuwa sare ya bao 1-1.
Ahly ndiyo klabu yenye mafanikio katika michuano hiyo mikubwa ya klabu Afrika, imebeba taji hilo mara nane wakati Pirates imefanya hivyo mara moja tu, mwaka 1995.

No comments:

Post a Comment