Thursday 21 November 2013

JK awapandisha vyeo makamishna 77 Polisi

Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete amewapandisha vyeo maofisa 77 wa Jeshi la Polisi kutoka Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) kuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP).
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Msemaji wa jeshi hilo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Advera Senso imesema waliopandishwa vyeo ni pamoja na makamanda wa polisi wa mikoa mbalimbali nchini. 
Aliwataja baadhi ya maofisa hao kuwa ni Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Ahmed Msangi, Kamanda wa Polisi  wa Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo na Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi.
Makamanda wengine waliopandishwa vyeo na mikoa yao kwenye mabano ni Diwani Athumani (Mbeya), Frasser Kashai (Kigoma), Geofrey Kamwela (Singida), Faustine Shilogile (Morogoro), David Misime (Dodoma) na Ferdinand Mtui (Mara).
Wengine ni Costantine Massawe (Tanga), Leonard Paul (Geita),  Ulrich Matei (Pwani), Evarist Mangala (Shinyanga)  Deusedit Nsimeke (Ruvuma), Fulgence Ngonjani (Njombe), George Mwakajinga (Lindi) na Dhahiri Kidavashari (Katavi).
Wengine ni baadhi ya makamanda wa vikosi, wakuu wa vitengo, Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi na Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam.
Mara ya mwisho kwa maofisa wa jeshi hilo kupandishwa vyeo ilikuwa Mei mwaka kuu wakati makamishna wawili na manaibu kamishna 19 walipoteuliwa.
Miongoni mwa walioteuliwa walikuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar e Salaam, Suleiman Kova na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi, Isaya Mngulu walipopandishwa cheo kutoka Naibu Kamishna (DCP) na kuwa Kamishna wa Polisi (CP).
Miongoni mwa waliopandishwa vyeo na kuwa manaibu kamishna wa Polisi ni Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, Thobias Andengenye na Michael Kamuhanda.

No comments:

Post a Comment