Friday 15 November 2013

Kaseja ampigia simu Barthez

SAA chache kabla ya kusaini mkataba wa kuichezea Yanga, Juma Kaseja alimpigia simu kipa wa Yanga, Ali Mustapha ‘Barthez’ na kumueleza kuhusu mchongo mzima wa klabu hiyo ya Jangwani kumuhitaji.
Barthez baada ya kupokea simu hiyo na kusikiliza alichoambiwa na Kaseja akamjibu; “Njoo tufanye kazi ndugu yangu.”
Kwa mujibu wa Barthez, hata kabla ya dili hilo, mara kwa mara huwa anawasiliana na Kaseja kuelezana mambo mbalimbali ya kimaisha hivyo hakuona ajabu kupokea simu ya kipa mwenzake.
“Unajua Kaseja huwa tunawasiliana mara kwa mara na hata alipotaka kusaini Yanga alinipigia kunielezea jambo hilo na mimi nikamjibu aje tufanye kazi pamoja hakuna tatizo,” alisema Barthez.
Barthez alisema kimsingi haoni tatizo kwa Kaseja kujiunga na Yanga kwani anaamini kila mmoja anaweza kucheza kwa nafasi yake huku mazoezi yakiwa ni silaha kubwa kwao.
“Tupo watatu hapa, kila mmoja anataka kucheza hivyo ni jukumu letu kujituma katika mazoezi na atakayeonekana kuwa bora ndiye atakayecheza hivyo sina shaka juu ya nafasi yangu,” alisema Barthez, ambaye yumo katika kikosi cha Taifa Stars.
Ujio huo wa Kaseja unaifanya Yanga kuwa na makipa watatu sasa katika kikosi chake wengine wakiwa ni Barthez na Deogratius Munishi ‘Dida’ ambao wote kwa pamoja wamewahi kuwa makipa wa Simba.
Kaseja amesajiliwa kwa dau la Sh 40 milioni na mkataba wake utadumu kwa miaka miwili.

No comments:

Post a Comment