Monday 11 November 2013

DCI Manumba astaafu

MKURUGENZI wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba, amestaafu kulitumikia Jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria baada ya kutimiza umri wa miaka 60.
Taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na kusainiwa na msemaji wake, SSP Advera Senso, inaeleza kuwa kabla ya kustaafu kwake Kamishna Manumba alilitumikia jeshi kwa nafasi mbalimbali kuanzia alipoajiriwa.
Senso alisema kuwa wakati mchakato wa kumpata mkurugenzi mpya wa nafasi hiyo ukiendelea, mkuu wa ufuatiliaji na tathmini CID makao makuu, Kamishna Isaya Mungulu, atakaimu nafasi hiyo kwa muda.
Nafasi alizowahi kushika ndani ya jeshi ni pamoja na kuwa mpokea mashtaka katika chumba cha mashtaka (1976-77), Mwendesha Mashtaka Wilaya ya Kibondo na Kasulu mkoani Kigoma (1977–1984).
Amekuwa pia mkufunzi katika Chuo cha Polisi Dar es Salaam (1984-1987), Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Magomeni na Kinondoni na Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam (1987–1993).
Manumba pia amewahi kuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Arusha (1993–1995), Mkufunzi Mkuu wa Chuo cha Polisi Moshi (1995 – 1996), Mkuu wa kitengo cha ‘Fraud’ makao makuu ya upelelezi (1996–1997), Mkuu wa kitengo cha usalama wa nchi, intelijensia na dawa za kulevya makao makuu ya upelelezi (1997–2001).
Amekuwa pia msaidizi wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (2001–2006), kisha mkurugenzi kamili wa makosa ya jinai.

No comments:

Post a Comment