Thursday 14 November 2013

Kichapo cha Arsenal champonza shabiki Uganda


KAMPALA, UGANDA
ARSENAL imemponza shabiki wake wa Uganda ambaye amepoteza nyumba baada ya kucheza kamari akiamini kwamba kikosi hicho kingeichapa Manchester United katika mchezo wa Ligi Kuu England uliofanyika Jumapili iliyopita.
Shabiki huyo anayeishi Wilaya ya Iganga Kaskazini mwa Uganda, kwa sasa anahaha kutafuta makazi ya kuishi na familia yake baada ya kupoteza nyumba hiyo kufuatia kichapo cha bao 1-0 ilichopata timu yake hiyo anayoishabikia katika mechi iliyofanyika Uwanja wa Old Trafford. Straika wa zamani wa Arsenal, Robin van Persie, ndiye aliyeifungia Manchester United bao hilo.
Kabla ya mechi ya miamba hiyo, shabiki huyo, Henry Dhabasani,  alicheza kamari kwa kuweka nyumba yake ya vyumba viwili dhidi ya Rashid Yiga kwamba Arsenal itashinda mchezo huo, taarifa hiyo ni kwa mujibu wa gazeti la Observer la Uganda.
Kwa upande wake, Yiga aliweka gari yake mpya Toyota Premio pamoja na mke kwamba Manchester United ingeshinda.
“Wawili hao waliweka ubishi wao huo kwenye maandishi, mbele ya viongozi wa kijiji na mashahidi wengine ambao ni wapenzi wa mpira wa miguu,” limebainisha gazeti hilo.
Dhabasani ana wanawake watatu na watoto watano na alizimia mwishoni mwa mechi baada ya timu yake ya Arsenal kunyukwa bao hilo 1–0.
Siku iliyofuata, mashabiki wa Manchester United walivamia nyumbani kwa Dhabasani na kumtoa na familia yake.

Mwanaspoti

No comments:

Post a Comment