Monday 11 November 2013

Hassanol apangua kesi ya kwanza


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jana Jumatatu ilimwachia huru Mwenyekiti wa Chama cha Soka Pwani (Corefa), Hassan Othman ‘Hassanol’ (45).
Hata hivyo Hassanol anaendelea kusota mahabusu akikabiliwa na kesi nyingine ya kukutwa na pembe za ndovu.
Pamoja na Hassanol wengine walioachiwa na mahakama hiyo  ni mfanyabiashara wa madini, Najim Msenga na Wambura Mahega baada ya kuwaona hawana hatia katika mashitaka matatu yaliyokuwa yakiwakabili likiwamo la wizi wa shaba yenye thamani ya Sh 333 milioni.
Najim ambaye ni mfanyabiashara wa madini na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, aliishukuru mahakama kwa kutenda haki, kuangalia ukweli huku akidai kwamba tangu azaliwe hajawahi kuiba.
Akisoma hukumu hiyo, ambayo imeandaliwa na Hakimu Devotha Kisoka na kusomwa na Hakimu Sundi Fimbo, washitakiwa walikuwa wakikabiliwa na mashitaka matatu ya kula njama, kuiba na kupokea mali ya wizi.
Mali hizo ni tani 26.475 za madini aina ya shaba zenye thamani ya Sh333 milioni zilizokuwa zikisafirishwa kutoka Zambia kwenda Dar es Salaam, mali ya Kampuni ya Liberty Express Tanzania Limited.
Hakimu Fimbo alisema ushahidi wa upande wa mashitaka haujathibitisha kama walikula njama kwa sababu hakuna mahali katika ushahidi huo unaoonyesha kuwa washitakiwa waliwahi kuwasiliana au kupanga njama ya kutenda kosa kwa njia yoyote ile.
Alisema dereva wa lori lililobeba shaba iliyoibwa angeweza kuwa shahidi lakini upande wa mashitaka haukumwita kueleza wapi shaba hiyo ilipelekwa kwa sababu ilitakiwa kupelekwa Kurasini lakini ikapelekwa kwenye yadi Bahari Beach.
Hakimu huyo pia alisema hakuna upelelezi uliowaonyesha washitakiwa hao wakiiba au wakipokea hizo shaba.
Kwa upande wa Najim wakati wa tukio hakuwepo, Dar es Salaam alikuwa Tanga kwenye msiba na upande wa mashitaka haukuwa na shida na hilo na kwamba yadi ni yake na yadi hiyo ina meneja ambaye ameajiriwa lakini upande wa mashitaka haukumwita kuwa shahidi.
“Kutokana na ushahidi huo pamoja na utetezi wa washitakiwa,  mahakama inawaona hawana hatia wapo huru,’’ alisema hakimu.

Mwanaspoti

No comments:

Post a Comment