Monday 11 November 2013

Van Persie aiua Arsenal tena Old Trafford


MANCHESTER United imeitia adabu Arsenal kwa kuichapa bao 1-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uliofanyika kwenye Uwanja wa Old Trafford jana Jumapili, shukrani kwa bao la kichwa na straika Robin van Persie katika kipindi cha kwanza.
Mdachi huyo alifunga katika dakika 27 na kuzima tambo za Arsenal huku Kocha David Moyes akimtambia mpinzani wake Arsene Wenger kutokana na kushindwa kumaliza uteja wa kuchapwa na Mashetani Wekundu.
Kichapo hicho kimeipunguza kasi Arsenal na sasa pengo la pointi dhidi yake na Manchester United limekuwa pointi tano.
Ushindi huo sasa umeifanya Manchester United kupanda kutoka nafasi ya nane hadi ya tano kwenye msimamo wa ligi baada ya kufikisha pointi 20 na sasa kuwa na uhakika wa kuendelea kuwamo kwenye mbio za kutetea ubingwa wao, huku Van Persie akiiua tena timu yake ya zamani baada ya kufanya hivyo msimu uliopita kwenye ushindi wa 2-1 kwenye uwanja huo huo wa Old Trafford.
Kwenye kipindi cha kwanza, Arsenal ilionekana kubanwa na kuchapwa bao hilo kabla ya kipindi cha pili kuingia kwa kasi kusaka bao la kusawazisha, huku Manchester United ikipata pigo mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya beki na nahodha wake Nemanja Vidic kugongwa kichwani na hivyo kulazimika kukimbizwa hospitali.
Kwenye kipindi cha kwanza kipa wa Arsenal, Wojciech Szczesny ndiye aliyepata misukosuko baada ya kuokoa shuti la umbali wa mita 25 lililopigwa na Wayne Rooney, licha ya kwamba shuti hilo lilipunguzwa makali kidogo kwa kumgonga mchezaji mmoja wa Arsenal.
Dakika za mwanzo, Manchester United iliyokuwa nyumbani Old Trafford ilimiliki mpira kwa asilimia 66 licha kwamba ilishindwa kutengeneza nafasi za maana za kufunga.
Mechi nyingine za ligi hiyo, Tottenham Hotspur ikiwa nyumbani White Hart Lane ilikubali kipigo kutoka kwa Newcastle United cha bao 1-0, huku Sunderland ikiiduwaza Manchester City kwa kuichapa 1-0 na Swansea City ikitoka sare na Stoke City kwa kufungana mabao 3 - 3.

No comments:

Post a Comment