Saturday 16 November 2013

Operesheni safisha TFF kuendelea mwezi ujao

WIKI chache baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah, kupewa likizo ya malipo, zoezi hilo linatarajiwa kuendelea ndani ya shirikisho hilo na kubakikiza watu wanne pekee.
Osiah, alipewa likizo ya malipo siku chache baada ya uongozi mpya kuingia madarakani chini ya Rais Jamal Malinzi aliyembwaga mpinzani wake, Athuman Nyamlani, kwa kura 73-52 katika kinyang’anyiro hicho.
Habari za uhakika kutoka ndani ya shirikisho hilo ziliipasha Tanzania Daima kuwa asilimia 99.8 ya wafanyakazi waliopo sasa wataondolewa, kwani kunahitajika kufanya kazi na watu wengine tofauti na hao.
Mtoa habari huyo aliyeomba jina lake kuhifadhiwa kwa kuwa sio msemaji wa TFF, alisema, fagio hilo litaendelea kusafisha mwezi ujao, ambapo sasa wamewaacha wapumue kutokana na kuwa na wasiwasi juu ya kuondoka kwao.
“Watu wengi wanamaliza mikataba yao mwezi ujao, tumeona tuwaache kwanza kidogo wamalize mikataba yao ila hatutaendelea na mtu na wengine pia wataondoka tu,” alisema mtoa habari huyo.
Aidha, chanzo hicho kilisema, ni asilimia 0.2 pekee ya wafanyakazi ambao wataendelea kufanya nao kazi wao kama uongozi mpya ili kufanya kile kilichowapeleka hapo cha kuendeleza soka na sio maneno kama watu wanavyosema mitaani.
Katika hatua nyingine, uongozi mpya umeendelea kuomba taarifa za kibenki lakini hadi jana bado walikuwa hawajapewa, licha ya Rais aliyemaliza muda wake Leodegar Tenga kukabidhi ofisi wiki kadhaa zilizopita.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment