Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema baadhi ya wabunge walitoa lugha za kuudhi dhidi ya tume hiyo katika Mkutano wa 13 wa Bunge uliomalizika juzi mjini Dodoma.

Akizungumza katika mahojiano maalumu nyumbani kwake Oysterbay, Dar es Salaam jana, Jaji Wariona aliwataka kutoingilia majukumu ya tume hiyo.

“Wabunge wasijiingize vinywani mwetu na katika akili zetu. Wapo waliosema kuwa sisi (Tume) siyo wataalamu pekee wa masuala ya Katiba…

Katika maandalizi yetu hatukufikiria wala hatukutaka kuwa wabunge. Tuliona kazi yetu ni kutoa ufafanuzi na uamuzi utakuwa wa Bunge, tulitegemea kuwa tutatoa ufafanuzi katika Kamati za Bunge, siyo Bunge la Katiba.”

Katika mkutano huo, wabunge walipitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013, baada ya kufanyiwa marekebisho kwa baadhi ya vifungu vilivyokuwa vikilalamikiwa, kikiwemo cha wajumbe wa tume hiyo kutoingia kwenye vikao vya Bunge la Katiba.

Katika mjadala wa muswada huo, baadhi ya wabunge walisema kuwa hakuna ulazima wa tume hiyo kuwepo katika Bunge hilo, huku baadhi yao wakieleza kuwa wajumbe wa tume hiyo siyo wataalamu pekee wa masuala ya Katiba.

“Wasije wakasema tume ina lake jambo katika Sheria ya Marekebisho ya Katiba. Wabunge ndiyo walitengeneza sheria hiyo, pia wanajua sababu za awali kutupa jukumu kwenye Bunge la Katiba na Kura ya Maoni na baadaye kutuondoa.”

Jaji Warioba alisema hivi karibuni wanasiasa wamediriki kusema wazi kuwa baadhi ya wajumbe wa tume hiyo hawana uwezo na wanalipwa fedha za bure.

“Kila mjumbe ana umuhimu wake, kauli ninazozungumza ndiyo msimamo wa Tume, ndani ya tume hii kila mtu ana umuhimu wake,” alisema.

Akizungumzia Bunge la Katiba, Jaji Wariona alisema ili kufanikisha kazi hiyo ya kihistoria kwa Taifa, wabunge wote hawana budi kuwa kitu kimoja na kuweka mbele masilahi ya taifa.

Amkumbuka Dk Mvungi

Akizungumzia hali ya Mjumbe wa Tume hiyo, Dk Sengondo Mvungi ambaye yuko Afrika Kusini kwa matibabu baada ya kujeruhiwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake wiki moja iliyopita, Jaji Warioba alisema wameelezwa kwamba anaendelea vizuri.