Friday 15 November 2013

NGUVU YA UMMA CHADEMA YASHINDWA KUMUOKOA MBUNGE WAKE ALIYETUPWA JELA SIKU 14

 
UTARATIBU wa Chadema kutumia kinachoitwa ‘nguvu ya umma na vurugu’ kushinikiza sheria ipindishwe kwa maslahi yake, umekwama kumnusuru Mbunge wa Ukerewe, Salvatory Machemli anayetumikia adhabu ya kukaa jela kwa siku 14.

Jana Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Chadema, Sylvester Masinde, alikiri kuwa nguvu ya umma iliyodaiwa kutumika kumnusuru Machemli, ni upotoshaji na hali ilivyokuwa, mamlaka zilishajiandaa kukabiliana nao.

Kutokana na hali halisi, Masinde alisema chama hicho hakiwezi na wala hakina mpango wa kutumia nguvu ya umma, kushinikiza Machemli atoke mahabusu.

Masinde alifikia hatua ya kuwambia viongozi wa ngazi ya msingi wa chama hicho kuwa ni vema utaratibu uliowekwa kisheria uheshimiwe.

Kiongozi huyo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, alisema suala hilo limechunguzwa na kubaini ni kweli Machemli aliruka dhamana, hivyo Mahakama Kuu pekee ndiyo yenye mamlaka ya kutengua uamuzi huo.

Machemli anakabiliwa na kesi ya uchochezi na Novemba 6 aliamriwa na Mahakama ya Wilaya kwenda rumande kwa siku 14, baada ya kuidharau kwa kutotokea wakati kesi ikiitwa.

Tofauti na ilivyokuwa kwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ambaye alisema lupango ndiko kwenye wapiga kura wake, kwa Machemli Chadema imeamua kufuata utaratibu kumtoa.

Kabla ya kuahirisha kesi hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Faustine Kishenyi aliagiza mbunge huyo baada ya siku 14 afikishwe tena mahakamani hapo akiwa na wadhamini wengine watatu ambao kila mmoja atatakiwa kuwa na hati ya nyumba.

Mamlaka zajiandaa Katika hatua nyingine, kiongozi huyo wa ngazi ya juu wa Chadema alikiri kuwa mamlaka wilayani humo, zilishajiandaa kukabiliana na nguvu ya umma.

Alidai alifuatana na viongozi wengine wa chama hicho kwenda kumjulia hali mbunge huyo, lakini barabarani walikuwa wakifuatwa kwa karibu na gari la Polisi. Hata hivyo, walipofika gerezani, walitakiwa na Mkuu wa Gereza waondoke.

Akizungumzia sababu za kuzuiwa kuingia gerezani hapo, kiongozi huyo alidai anahisi pengine mamlaka husika zilitishwa na uvumi usio wa kweli kuwa zingetumika nguvu za umma kushinikiza Mahakama itoe dhamana kwa mbunge huyo.

Hata hivyo, Mkuu wa Magereza wa Wilaya, Edward Nyabange, alisema viongozi hao wa Chadema wakiwa zaidi ya 10 walizuiwa kuingia gerezani hapo kwa sababu ya kutofuata utaratibu.

Alisema utaratibu uliopo unaelekeza Jumapili pekee ndiyo mahabusu na wafungwa wanaruhusiwa kutembelewa na jamaa zao na kuongeza kuwa mbali na viongozi hao kuvunja utaratibu, pia idadi yao ilikuwa kubwa.

-Habari leo


No comments:

Post a Comment