Saturday 16 November 2013

Yanga yasajili kifa, yaitibulia Simba


UONGOZI wa Yanga ambao haukosekani kwenye mazoezi ya Taifa Stars yanayoendelea katika Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam imepiga bao jingine la maana kwa watani zao wa Msimbazi.
Imemsainisha kiungo mshambuliaji matata, Hassan Dilunga aliyetamba na Ruvu Shooting msimu huu ikiwa ni usajili wa pili katika dirisha dogo baada ya kumsainisha Juma Kaseja.
Agosti mwaka jana mmoja wa viongozi wazito aliyejiuzulu Simba, alimalizana na Dilunga na akapeleka jina lake kwenye Kamati ya Usajili ya klabu hiyo akiahidi kumlipa kila kitu mpaka mshahara kwa fedha yake ya mfukoni, lakini jopo hilo likamkataa mchezaji kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kutaka kumkomoa kiongozi huyo.
Dilunga, ambaye alikulia kwenye timu ya vijana ya Ruvu Shooting, ni kiungo mshambuliaji na fundi aliyetamba kwenye mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara ambaye kwa mujibu wa mchambuzi maarufu wa soka, Edo Kumwembe Yanga imepata mchezaji wa maana na ambaye atakuwa na madhara kwa timu pinzani.
“Nimemfuatilia sana kwenye ligi ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kutawala kiungo, kukokota na kupenya anavyotaka, anatumia sana akili kuliko nguvu, mwepesi kugeuka halafu ana kasi nzuri, ni fundi wa pasi za mwisho na anajua kufunga mabao,”alisema Edo.
Mwenyekiti wa Kamati ya usajili wa Yanga, Abdallah Bin Kleb ambaye habanduki kwenye mazoezi ya Stars, alithibitisha jana
Ijumaa kwamba wamemsainisha mchezaji huyo mkataba wa miaka mitatu ingawa Kocha wa Ruvu, Boniface Mkwasa alishtuka na huenda akakosa raha wikiendi hii yote kwavile
Yanga wamemgusa pabaya.
Simba na Azam FC zilikuwa zikimnyatia mchezaji huyo, lakini Yanga ikawazidi ujanja.
Abdallah Bin Kleb alisema; “Tunaendelea na harakati zetu za kuboresha timu, kama nilivyosema awali malengo yetu ni kupata timu iliyo bora Tanzania na Afrika, tulimsajili Juma Kaseja na sasa Hassan Dilunga. Tumemsainisha mkataba wa miaka mitatu na kuanzia sasa ni mchezaji wetu halali.”
Mwenyekiti wa Ruvu Shooting, Kanali Charles Mbuge alisema: “Kwa sasa niko mbali kijijini kwetu Musoma nimepumzika, sina taarifa hizo kwa undani.” Hata hivyo, Mbuge aliongeza kuwa, Dilunga alikuwa bado ana mkataba wa miaka mitatu na Ruvu.

Mwanaspoti

No comments:

Post a Comment