Thursday 21 November 2013

Tajiri Simba awafuata Yondani na Msuva


KIGOGO mmoja mwenye ushawishi mkubwa Simba na anayewania kugombea uongozi mwakani (jina tunalo), ameanza mazungumzo ya faragha na wachezaji wawili wa Yanga.
Wachezaji hao ambao mikataba yao inamalizika ndani ya miezi sita ijayo ni beki kisiki, Kelvin Yondani na winga mwenye kasi, Simon Msuva.
Habari za ndani ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba kiongozi huyo amepanga kuwasainisha wachezaji hao ambao kuanzia mwezi ujao kikanuni watakuwa huru kufanya mazungumzo, kama sehemu ya kampeni zake kwenye uchaguzi huo.
Yondani aliondoka Simba misimu miwili iliyopita na kusababisha madhara kwenye safu ya ulinzi ya Wekundu hao wa Msimbazi kwani wamekuwa wakikosa mbadala makini, ingawa kurejea kwa Joseph Owino na usajili wa Gilbert Kaze vimewapa ahueni.
Mwanaspoti linajua kuwa Yondani na Msuva ingawa wamegoma kukiri lakini wamekuwa wakishawishiwa na kigogo huyo wa Simba na wameelekea kuridhia ndio maana hawajataka kupaparika kufanya mazungumzo mapya na Yanga.
Msuva ambaye alijiunga na Yanga akitokea Moro United iliyoshuka daraja amekuwa kwenye fomu kwa kipindi kirefu na jana Jumatano alisema: “Nimebakiza muda wa miezi sita katika mkataba wangu na Yanga, kisheria sina kipingamizi cha kufanya mazungumzo na timu yoyote kuhusu hatma yangu ya soka, ila bado sijazungumza na Yanga kuhusiana na suala la kuongeza mkataba mpaka sasa, nasubiri kumalizia mkataba wangu na Yanga, endapo watafuata yale ninayoyataka, haitakuwa shida kuendelea kuichezea Yanga, lakini kama itakuwa kinyume, itakuwa tofauti.”
Yondani kwa upande wake alisema mkataba wake unamalizika mwakani mwezi Mei na suala la kuongeza mkataba litatokana na makubaliano baina yake na timu yake ya sasa na hata timu nyingine itakayomuhitaji.
“Mkataba wangu unamalizika baada ya msimu huu, kwa sasa nipo huru kufanya maandalizi ya kazi yangu kwa kufanya mazungumzo na timu zozote, ila kusaini Yanga nahitaji kupata muda wa kutafakari na kama watafuata masharti yangu nitakubaliana nao,” alisema Yondani bila kufafanua ni masharti yapi wala hakukiri kufuatwa na Simba.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Yanga, Abdallah Bin Kleb ambaye mara kadhaa amekuwa akiigaragaza Simba katika vita ya kuwania mchezaji, alisema kuwa hawajafanya mazungumzo na Yondani na Msuva lakini hawana papara kwavile bado ni mali yao mpaka mwisho wa msimu.
“Msuva na Yondani ni wachezaji wetu, bado wana mkataba na sisi na si siri kwa kipindi ambacho wamebakiza tunajipanga kujua tunafanya nini kwao, muda ukifika tutawajulisha, hatuna papara katika usajili, tunachofanya sasa ni kusaka straika wa kigeni kutoka nje,” alisema Bin Kleb kwa kujiamini huku akionyesha kutokuwa na presha ya kuwapoteza wachezaji.
Habari za ndani zinadai kwamba baadhi ya wanachama maarufu wa Simba wameanza mikakati ya chinichini kujipanga kuwania uongozi wa juu klabu hiyo kwenye uchaguzi utakaofanyika baada ya kumalizika kwa ligi mwakani.

Mwaspoti

No comments:

Post a Comment