Saturday 26 October 2013

Chadema kuwasha moto Bunge lijalo


Chama cha Chadema kimeonya kuwa moto utawaka kwenye kikao cha Bunge kinachoanza wiki ijayo, iwapo wabunge wa CCM wenye msimamo wa kihafidhina watakwamisha marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iliyozua tafrani Bunge lililopita.
Akifungua mkutano wa baraza la uongozi la Chadema Kanda ya Kaskazini jijini Arusha jana, Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe alisema wabunge wa Chadema wanakwenda Dodoma wakiwa wamejiandaa kupigania marekebisho ya sheria hiyo.
“Katika hili tutashirikiana na wabunge wote wa vyama vyote wenye mapenzi mema wakiwemo wale wa CCM,ili kuhakikisha Taifa linapata katiba bora” alisema Mbowe.
Alisema msimamo wa kupigania mabadiliko hayo bungeni unachagizwa na makubaliano yaliyofikiwa wakati wa mazungumzo kati ya vyama vya siasa na Rais Jakaya Kikwete, lakini akaonya kuwa hawatasita kuhamishia mapambano hayo nje ya bunge kwa kushtaki kwa umma iwapo hoja zao za msingi zitapuuzwa.
Rais Kikwete asikubali kutishiwa
Akizungumzia taarifa za kuwepo mkakati wa kukwamisha marekebisho hayo miongoni mwa baadhi ya wabunge wa CCM, Mbowe alimshauri Rais Jakaya Kikwete kutokubali kutishiwa na wabunge wachache wanaoogopa mabadiliko.
“Wabunge wachache wanaotishia kukwamisha marekebisho hayo hawako tayari kushuhudia Rais Kikwete akilivunja bunge kwa sasa kama katiba inavyoelekeza, sababu wanaogopa uchaguzi kutokana na kutokuwa na uhakika wa kurejea bungeni,” alisema Mbowe
Alishauri marekebisho ya sheria hiyo iliyotiwa saini na Rais Kikwete Oktoba 10, mwaka huu lisiwe suala la majadiliano bali yawe ni maagizo na maelekezo kutoka kwa Rais ambaye anapaswa kutumia madaraka yake ya kikatiba kutimza lengo lake jema.
“Nashangazwa Rais Kikwete kukubali kutishiwa hata na baadhi ya mawaziri aliowateua yeye, katika jambo hili jema la kulipatia taifa katiba bora inayobeba maslahi ya Taifa kwa kuunganisha Watanzania wote bila kujali itikadi zao kisiasa wala makundi yao kijamii,” alisema Mbowe.

Chanzo Mwananchi

No comments:

Post a Comment