Friday 25 October 2013

Kaseja ampigia simu Barthez

KIPA wa zamani wa Simba, Juma Kaseja, amempigia simu kipa namna moja wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’ na kumuambia maneno kadhaa ya kiutu uzima.
Kaseja ambaye aliachwa Simba kwa kisingizio cha kuporomoka kwa kiwango chake, amempigia simu Barthez na kumueleza kwamba anatakiwa kuwa mvumilivu sana katika suala la mpira wa Tanzania.
Barthez alikuwa kipa mbadala wa Kaseja wakati wote wakiwa Simba, kabla ya yeye kuhamia Yanga ambako amefanikiwa kuwa kipa namba moja.
Chanzo cha uhakika kimeeleza, Kaseja aliamua kufanya hivyo baada ya kuona matatizo yaliyomkuta Barthez ya kuangushiwa mzigo, kwamba ndiye aliyesababisha Simba kusawazisha mabao yote matatu na mechi kati ya timu hizo kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.
“Kaseja alikwenda (uwanja wa) Taifa siku ile, tangu pale alionyesha kuumizwa sana na Barthez kuangushiwa mzigo. Siku iliyofuata alimpigia simu na kumueleza kwamba anapaswa kuwa mvumilivu sana kwa kuwa mpira ndiyo kazi yake.
“Barthez alionyesha kufarijika na alimueleza Kaseja anavyoumia hasa kuhusiana na mabao yalivyotokea na mashabiki wasiokuwa makini wanavyomtwisha mzigo. Lakini inaonekana maneno hayo ya Kaseja, yamemsaidia sana,” kilieleza chanzo hicho. Kuhusiana na simu hiyo, Kaseja hakupatikana lakini Barthez hakupokea simu.
Hivi karibuni, mashabiki wa Yanga walivamia nyumbani kwa Barthez eneo la Chanika jijini Dar es Salaam wakitaka kumpiga kwa madai ndiye aliyechangia Simba kusawazisha mabao matatu katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Jumapili iliyopita.
Hata hivyo, wengi wenye utaalamu wa mpira wamekuwa wakikosoa tofauti na kueleza mabao hayo yalitokana na uzembe wa safu ya ulinzi na hasa mabeki.
Tayari kocha, Ernie Brandts ameshampumzisha Barthez katika mechi ya Yanga dhidi ya Rhino juzi na Deogratius Munish ‘Dida’ akapewa nafasi hiyo.

No comments:

Post a Comment